-

.

.

TRAMEPRO

TRAMEPRO

NAIPENDA NCHI YANGU TANZANIA

Wednesday 30 July 2014

KATIBA YATIKISA IDDI

Masheikh wayacharukia makundi yanayovutanaPinda awasihi Ukawa warudi bungeni kuyamaliza
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa (kushoto), Makamu wa Rais Dk. Ghalib Bilal na Mufti Shaaban Bin Simba wakiswali swala ya Iddi el Fitr kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam jana. Picha/Omar Fungo
Mjadala kuhusu katiba mpya ulitawala katika hotuba mbalimbali zilizotolewa jana wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya Iddi El Fitri jana huku masheikh na viongozi wa serikali wakiwataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutumia weledi, uadilifu na kuepuka maslahi binafsi ili kuhakikisha Watanzania wanapata katiba iliyo bora.

SHEIKH MKOA WA IRINGA

Akizungumza baada ya kumalizika kwa swala ya Idd El-Fitri, iliyofanyika katika Uwanja wa Samora mjini Iringa jana, Sheikh wa Mkoa huo, Mohamed Mgwila, alisema viongozi wa dini wanashirikiana na waumini wote kuombea amani nchini kuhusiana na mchakato  wa katiba mpya ili maslahi ya umma yazingatiwe na siyo ya binafsi au ya chama.

“Viongozi wote wa dini hapa nchini tunahakikisha kuliombea taifa kupatikana kwa katiba iliyo sahihi bila kuvuruga amani iliyopo,” alisema Sheikh Mgwila.

Alisema siyo jambo jema kwa wahusika, hususan viongozi wanaoshughulikia jambo hilo  kujikita katika kutetea maslahi ya kundi au watu fulani katika jamii, bali inatakiwa watetee maslahi ya umma, ambayo itawasaidia kizazi hiki na kijacho.

MDHAMINI WA BAKWATA
Mdhamini wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Omary Nzowa,  alisema maadhimisho ya Sikukuu ya Idd El-Fitri yanapaswa kuimarisha ushirikiano   miongoni mwa jamii, huku akitaka kila kundi kutumia hekima hiyo kurejesha uhusiano wao.

ISLAMIC CENTRE
Mkuu wa Kituo cha Islamic Centre, Sheikh Hassan Mohamad, aliwataka  Waislamu kutoacha ibada hata baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

SHEIKH MKOA DODOMA
Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu Shabani, amewataka wajumbe wa Bunge hilo kuwa kitu kimoja na kuacha kuendekeza makundi na malumbano ya kisiasa yasiyo kuwa na msingi wakati watakaporudi bungeni mapema mwezi ujayo ili kupata katiba iliyo bora na siyo bora katiba.

Alisema hayo alipokuwa akihutubia waumini wa dini ya Kiislamu kwenye swala ya Idd El-Fitri, iliyosaliwa katika Msikiti wa Gadafi mjini Dodoma jana.

Sheikh Rajabu alisema wajumbe wa Bunge hilo wamekuwa wakiendekeza malumbano yasiyokuwa na tija kwa kila mmoja kusimamia maslahi ya chama chake na kuacha kuwa wamoja katika kuhakikisha wanapata katiba iliyo bora.

“Kama sintofahamu hii haitakwisha, basi ni ukweli usiopingika kuwa hakuna katiba itakayopatikana kutokana na kutokuwapo kwa umoja wa wajumbe wa Bunge hili la Katiba,” alisema Sheikh Shabani.

Aliwataka wajumbe hao kutambua kuwa wao ni wawakilishi wa wananchi, hivyo hawana budi kufanya maamuzi kwa kulenga maslahi ya wananchi na siyo vyama vyao.

“Katiba hii siyo kwa ajili ya chama fulani wala kikundi fulani, hivyo tunatakiwa kuwa makini na kuwaombea wajumbe hawa ili waweze kuachana na malumbano ya vyama na kufanya kile walichotumwa na wananchi,” alisema.

Aliwataka Waislamu kote nchini kuendelea kuliombea taifa kuwa na utulivu na wasiwe tayari kurubuniwa ili wawe chanzo cha uvunjifu wa amani iliyopo nchini.

Hata hivyo, aliwasihi waumini wa dini hiyo kuutumia mfungo wa mwezi wa Ramadhani kuwa semina kwao ya kufanya mambo mema siku zote za maisha yao.

“Siyo leo Ramadhani inaisha basi iwe ndiyo tumefungulia maovu yetu tuliyoyaficha katika mwezi, ambao umeonekana kuwa na utulivu wa hali ya juu baa zimekuwa na utulivu kana kwamba sisi Waislamu ndiyo inaoneka tumekuwa wanywaji sana,” alisema.

SHEIKH ZUBERI
Sheikh Ahmed Zuberi aliwataka Watanzania kuendelea kuijenga na kuilinda amani isichafuliwe na wanasiasa, ambao watapita na vyama vyao vitapita.

Aliwataka wanasiasa kuchunga kauli zao wanazozitoa kwa wananchi wakati wakiongea nao, kwani zinaweza kuleta machafuko.Alisema maeneo yenye machafuko kwa sasa katika maeneo mengi yanasababishwa na watu kutaka madaraka kwa nguvu hata kufikia wakati kuvunja amani iliyopo.

SHEIKH WILAYA DODOMA

Sheikh wa Wilaya ya Dodoma, Mohamed Ramadhani aliwataka Waislamu nchini kudumisha amani wakati wote na kuepuka ushawishi kutoka kwa watu wasioitakia mema nchi

Akizungumza mjini Dodoma katika swala ya Idd El-Fitri, iliyofanyika kiwilaya katika Msikiti wa Jailan, Sheikh Ramadhan alisema Watanzania wamepewa neema na Mwenyezi Mungu ya amani, ambayo nchi nyingine ulimwenguni hazina.

“Watanzania wenzangu tuendeleze amani yetu tuliyonayo. Wote Wakristo kwa Waislamu tujiepushe na vurugu, ambazo zinaweza kuiingiza nchi yetu katika machafuko ili kuendelea na amani na kufanya vitu kwa uhuru popote tutakapotaka kwenda bila kupata tabu yoyote ya vurugu,” alisema Sheikh Ramadhani.

Alisema Watanzania wanatakiwa kuilinda amani na kujiepusha na vurugu na ushawishi, ambao wamekuwa wakipatiwa na watu wengine.Aliwataka Watanzania kujitahidi kuimarisha amani na hasa wakati huu nchi ikiingia katika mchakato wa katiba mpya.

Alisema waasisi wa taifa walijenga taifa katika hali ya umoja hivyo Watanzania wanapaswa kuutunza umoja huo uliopo na kuendelea kuishi kwa amani kama miaka yote.

“Nchi kama haina amani, wananchi wake watashindwa kuwa na uhuru wa kuabudu kama tunavyoabudu hivi sasa ni kwa sababu ya amani tuliyo nayo. Tukiipoteza kuirudisha kwake itakuwa ni shida,” alisema Sheikh Ramadhan.

Aliongeza: “Waislamu na Wakristo tumekuwa tukishirikiana kwa miaka mingi sana na tumeimarisha amani yetu tukiwa pamoja hata katika mazingira tunayoishi tunaishi tukiwa katika mchanganyiko hata mtume aliishi na watu wasio Waislamu.”

Aliwataka Waislamu kote nchini kuendeleza kutenda mema kama walivyokuwa katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani ili baraka za Mungu ziendelee kuwa nao.

SHEIKH MKOA RUKWA
Sheikh wa Mkoa wa Rukwa, Rashid Akilimali, aliwashauri wajumbe wa Bunge hilo wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kurejea bungeni ili kuijadili rasimu ya katiba.

Alitoa ushauri huo mara baada ya kumalizika kwa sala ya Iddi El-Fitri, iliyofanyika kimkoa, katika Msikiti Nuru, maarufu kwa jina la “Bakwata”, uliopo katika Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.

Alisema ifike mahala Ukawa waamini kuwa kile wanachokifanya siyo sahihi kutokana na kususa kuhudhuria vikao vya Bunge hilo.
Sheikh Akilimali alisema kitendo hicho kinasababishia serikali na wananchi hasara kubwa kutokana na kutopata katiba kwa wakati, huku fedha nyingi zikiwa zimetumika.

IMAMU WA MSIKITI WA NURU
Awali, akitoa mawaidha katika ibada hiyo ya Idd, Imamu wa Msikiti huo, Nassibu Masoud, aliwataka vijana wote nchini kumrudia Mungu na kuachana na mambo ya kidunia na yale ya kuiga, ambayo wengi wao yamekuwa yakiwasababishia madhara makubwa.

Alisema kwa sasa vijana wengi wanakosa kuishi kwa maadili kutokana na kujiingiza katika mambo yasiyofaa na kuacha kumcha Mwenyezi Mungu.

SHEIKH MKOA ARUSHA
Viongozi wa dini ya Kiislamu mkoani Arusha wameahidi kuendelea kusaidia kutoa  ushirikiano wa kukabiliana na watu wanaopitia migongo ya madhehebu ya dini kufanya  maovu na kuwataka vijana kuwa macho na baadhi ya watu wanaotaka kuwarubuni  wakubali kutumia nguvu zao kuvuruga amani ya nchi.

Wakizungumza baada sala ya Idd El-Fitri, viongozi  hao, akiwamo  shekh  mkuu  wa  mkoa  Shaban  Bin  Jumaa, wamesema  kimsingi  wote  wanaofanya  maovu  kwa  kupitia   kwenye  madhehebu  ya dini   siyo  waumini  wa  kweli   kwani  hakuna dhehebu la  dini  linaloelekeza  mtu  kufanya maovu Shekh shabani  amesema  vitabu vyote  vitakatifu  vinaonyesha kuwa  lengo  la  madhehebu  yote ya dini  ni  kutenda  mema  na  kushirikiana  na  kupendana  na watu wote waliopokea  ujumbe  huo  vizuri  wamekuwa wanatekeleza  hilo   na  ni jambo lililoko wazi  kuwa  wanaokwenda kinyume   eidha  wana  agenda  zao   ama  hawajaelewa  vizuri   na  wanahitaji  kujifunza zaidi kwa upande wake  Imamu  wa  msikiti  wa  Ngarenaro  Mahamud  Suleiman  Nyambwa  na  Imamu wa Msikiti  wa  Ollmatejoo  Omari  Saidi   wameiomba serikali  kutomuonea  huruma  mtu yeyote  anayetaka kutumia  kivuli  cha  dini  kuvuruga  amani.

Viongozi  hao  wamesema   kimsingi  licha  ya  kuwapo  kwa  tofauti  za  njia  za  kuabudu  dini  zote  zinahamasisha amani upendo  na  ushirikiano  na  wanaokwenda kinyume  hawana lengo  la  kuabudu  bali  wanaweza  wakawa  na  agenda zao Sala  ya Idd El-Fitri,  ambayo kimkoa ilifanyika  katika  uwanja  wa  Sheikh  Amri  Abedi   na  pia  katika  misikiti mbalimbali   imemalizika  kwa  amani  na  huku  jeshi  la  polisi  likiwa  limeimarisha  ulinzi  wa  aina  mbalimbali   ukiwemo  wa  askari  kanzu  na  wa  kawaida.

SHEIKH MKOA RUVUMA
Waumini wa dini ya Kiislamu mkoani Ruvuma wametakiwa kusherehekea Sikukuu ya Idd El Fitri kwa amani, utulivu na upendo miongoni mwao na jamii inayowazunguka kama ilivyoagizwa na Mwenyezi Mungu katika mafundisho yake kwa wanadamu.

 Kauli hiyo ilitolewa na Shaban Kitete wa Mkoa wa Ruvuma wakati akitoa mawaidha kwenye Msikiti wa Mkoa wa Ruvuma uliopo mjini Songea katika kusherehekea Sikukuu ya Idd El Fitri.

Alisema Waislamu wote nchini wanapaswa kuwa chachu ya kudumisha amani, umoja na upendo uliopo nchini siyo tu wakati wa mfungo wa mwezi wa Ramadhan na Sikukuu ya Idd wanapaswa kuishi hivyo katika maisha yote.

Aidha amewataka kujijengea utamaduni wa kusherehekea sikukuu hiyo kwa kualika watu wengine bali kujali itikasi zao za kidini kwa kufanya hivyo kunadhirisha maana halisi ya sikukuu hiyo na kutazidisha upendo na usalama wa nchi ambao kila mmoja anauhitaji katika kuishi kwake na kamwe wasikubali kutumiwa watu au vikundi vya watu wasiotakia mema nchi iliyojaa amani na utulivu kwa miaka mingi.

Amesema kila Mtanzania amnapaswa kumshukuru Mungu kwa kuijalia amani nchi kwa miaka mingi hivyo kila mmoja anapaswa kuishi katika misingi ya kudumisha amani hiyo iliyopo ambayo ina historia kubwa ndani na nje ya nchi ambayo inamfanya kila mmoja ajivunie kuitwa Mtanzania ikilinganishwa na matukio ya uvunjifu wa amani yanayotokea katika mataifa mengine ulimwenguni ambayo yanasababisha vifo kila uchao.

Akitoa mfano wa maafa hayo Shekh Shaban Kitete amelitaja tukio la hivi karibuni ambalo ndege ya nchini Malasya imaeangushwa na kusababisha vifo vya takribani 300 ulimwengu wote umelaani na kukemea mauaji hayo lakini ulimwengu huo huo unashindwa kulaani na kukemea kwa nguvu mauaji yanayofanywa na Israel kwa wananchi wa Palestina ambayo mpaka sasa idadi yao inafikia zaidi ya mia moja.

Aidha ametoa wito kwa mataifa yote ulimwenguni kote kutumia nguvu zao kuhakikisha ulimwengu wote unakuwa salama na wenye amani na utulivu kwani muumini wa imani yoyote anayeweza kuabudu kama hakutakuwa na amani ya kuwafanya wanadamu wote kuishi kama ndugu bila kujali imani na itikadi walizo nazo kwa sababu imani zote zinamtukumza na kumuabudu Mungu mmoja.

Akizungumzia mchakato wa katiba mpya unaoendelea Shekh Shaban amewaasa wajunbe wa umoja wa katiba ya wananchi(UKAWA) kurejea bungeni kuendelea na mjadala huo ili hatimaye katiba mpya itakayowasaidia watanzania wote kuishi kwa amani na kujiletea maendeleo yao iweze kupatikana na amesema kuwa kama UKAWA wanasusia bunge hilo kwa maslahi na mustakabali mwema wa nchi Mungu awabariki lakini kama ni kwa maslahi yao binafsi na ya kisiasa Mungu atawahukumu.

Amewaasa wanasiasa wote chini kudumisha amani,upendo na utulivu kwa kutumia utamaduni wa kujadiliana na kuridhiana katika masuala yote yaliyo na utata kwa mustakabali wa nchi kama ulivyorithishwa kwa wazee wa taifa hili na siyo kulumbana na kukashifiana kwani huo siyo utamaduni wa watanzania.

PINDA
Akizungumza katika Baraza la Iddi lililofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam jana, Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliwasihi wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuacha kususia vikao vya Bunge la Katiba na kurejea bungeni ili wapate nafasi ya kuzungumza tofauti zao na kuzimaliza kwa nia ya kunusuru mchakato wa kuundwa kwa katiba mpya.

Akieleza zaidi, Pinda alisema kuwa kiutaratibu, ndani ya Bunge Maalum la Katiba kuna Kamati ya Mashauriano ambayo inaweza kumaliza mabishano au tofauti zozote zilizojitokeza baina yao.

Ukawa huwahusisha wajumbe wengi kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi.
Hii siyo mara ya kwanza kwa Waziri Mkuu Pinda kuwasihi wajumbe wa Ukawa kurejea bungeni.

Aliwahi pia kutoa kauli kama hiyo mkoani Kilimanjaro wakati akiweka jiwe la msingi katika Chuo cha Ufundi Gonja/Mheza, kilichopo katika Wilaya ya Same, akisisitiza kuwa ni vyema wakarejea na kuzungumza ili wasameheane pale walipokosea na kuwezesha mchakato wa kuundwa kwa katiba kuendelea.

Bunge hilo maalum la katiba linatarajiwa kuanza tena Agosti 5, lakini hadi sasa, uwezekano wa wajumbe wa Ukawa kurejea bungeni ni mdogo kwani viongozi wao, wakiwamo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na James Mbatia wa NCCR - Mageuzi wamekuwa wakisisitiza kuwa hawatarejea bungeni hadi watekelezewe masharti yao.
 
Ukawa waliamua kutoka bungeni na kuwaacha wajumbe wengi walio wafuasi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya kupinga jaribio la kubadili rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji mstaafu Joseph Warioba, ambayo imeonyesha kuwa maoni ya wananchi yakitaka muundo wa muungano wa serikali tatu.

Wajumbe wanaoiunga mkono CCM wamekuwa wakipinga maoni hayo ya Tume ya Warioba na kutaka kuendelea kuwapo kwa muundo wa muungano wa serikali mbili lakini uliofanyiwa mabadiliko makubwa.

Imeandikwa na Thobias Mwanakatwe (Dar), George Tarimo (Iringa), Paul Mabeja (Dodoma), Furaha Eliab (Mbeya), Juddy Ngonyani na Arafa Masingo (Sumbawanga), Asraji  Mvungi (Arusha), Rahma Suleiman (Zanzibar) na Natha Mtega (Songea).

0 comments:

Post a Comment

MWENYEKITI WA TRAMEPRO BWANA SIMBA ABDULRAHMAN SIMBA AKITOA SALAM ZA PONGEZI KWA MHE. DKT JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI KWA KUCHAGULIWA KUWA RAISI WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SEND EMAIL TO TRAMEPRO

Name

Email *

Message *