-

.

.

TRAMEPRO

TRAMEPRO

NAIPENDA NCHI YANGU TANZANIA

Sunday 28 September 2014

TIBA ASILI BADO IMEGUBIKWA NA CHANGAMOTO

   AGOSTI 31 mwaka huu kulikuwa na Maadhimisho ya Siku ya Tiba Asili ya Mwafrika yaliyofanyika Zanzibar katika viwanja vya Bustani ya Victoria mjini humo.
Moja ya mambo yaliyosisitizwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Mohamed Shein, kupitia hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, ni pamoja na kukemea baadhi ya watu kisiwani humo wanaojitangaza kupitia baadhi ya misikiti na mabaraza kuwa wana uwezo wa kutoa Tiba Asili, akisema kufanya hivyo ni kinyume na sheria.



Lakini pia hakusita kusema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inalipa kipaumbele suala la utafiti wa Tiba Asili na kuwa kuna uhusiano mzuri kati ya Wizara ya Afya na chama cha Watabibu Asili visiwani humo. Mwisho akaagiza mamlaka husika kushughulikia tatizo hilo.

Caroline mtafiti  wa tiba Asili kutoka chuo kikuu cha Berlin Ujerumani akipata maelezo kutoka kwa Mtabibu na Mtafiti wa Tiba Asili Bwana Boniventura Mwalongo ambaye pia ni Katibu wa ASSOCIATION OF TRADITIONA AND ALTERNATIVE MEDICINE IN EAST AFRIKA kutoka Tanzania  
Awali akisoma hotuba yake katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala Zanzibar, Mayassa Salum Ally Alisema kuwa Wizara ya Afya kupitia baraza hilo imefanya jitihada mbali mbali kuinua Tiba Asili na Tiba Mbadala na kufanikiwa kuongeza idadi ya wataalamu hao ambapo sasa kuna watabibu 193 waliosajiliwa na kuna jumla ya kliniki 18 na vilinge  125.

 Rais wa chama cha Tiba Asili na Tiba Mbadala Afrika Mashariki Lyidia Matoke Akitoa Maelezo kuhusu Tiba Asili Kwa Makamu wa Kwanza wa Rais  wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad

Sera ya Taifa ya Afya inaonyesha kuwa kabla ya Uhuru, huduma za afya zilikuwa zikitolewa zaidi katika maeneo ya shughuli za kiuchumi kama miji na mashanba makubwa. Baada ya Uhuru serikali iliweka msukumo zaidi katika kupanua huduma za afya ili kuwafikia wananchi walio wengi, hasa walioko maeneo ya vijijini.
Tiba Asili na Tiba Mbadala imekuwa ikishika kasi kila kukicha, japokuwa kuna changamoto za hapa na pale. Kuna haja ya kukubali kuwa changamoto nyingi zinazotokea katika eneo hili la Tiba Asili na Tiba Mbadala huenda zinatokana na ukosefu wa elimu ya kutosha kwa watanzania walio wengi ambao mara nyingi wamekuwa wakishindwa kutofautisha Tiba Asili na tiba nyingine zinazotolewa kwa kisingizio cha mtindo huo.
Kutokana na mkanganyiko huu, kumekuwa na tafsri za aina tofauti juu ya aina za waganga. Katika imani za kawaida, kuna aina tatu za waganga: Waganga wa Asili, Waganga wa Jadi na Waganga wa Kienyeji.
Kutokana na tafsiri inayotolewa na Chama Cha Utabibu Asili Tanzania (ATME),  Mganga wa asili ni yule anaye shughulika na tiba za maradhi kwa kutumia dawa za asili, kutibu maradhi  kwa binadamu, wanyama mimea kwa kufuata maadili ya utoaji huduma ya matibabu
Mganga wa Jadi: Anatumia Mila na Desturi katika tiba na utoaji dawa kwa wagonjwa iwe binadamu, wanyama, mimea. Hutegemea zaidi mila na desturi pamoja na tiba asili na dawa za asili kama kanuni na maadili ya utoaji huduma ya tiba.

Mganga wa kienyeji: Hana mafunzo maalumu ya tiba ya upande wowote wa tiba katika utoaji wake wa huduma kwa jamii. Ni mtu anayeweza kuchanganya taaluma mbalimbali hata za kisayansi ili mradi afanikishe alichokusudia. Mganga huyo pia anaweza kutumia vazi lolote liwe la Sheikh, Askofu, Daktari, Mganga wa Asili, ilimradi afikie lengo lake.

ATME wanasisitiza kuwa, mganga yoyote mwenye fani nzuri akiitumia katika kutenda maovu, huyo ndiye mganga wa kienyeji na wala si mtaalamu wa Tiba za Asili.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), takribani 60% ya wananchi huanza kutumia tiba asilia wanapopatwa na maradhi kabla ya kwenda vituo vya kutolea huduma za afya.
Nchini Tanzania Tiba Asili imekuwa na changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni ile ya baadhi ya watu kuihusisha na vitendo vya kishirikina, hali ambayo ni kinyume na sheria na taratibu zake, lakini pia kupotosha jamii.
Kwa mujibu wa Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala ya mwaka 2002, watabibu wote wa Tiba Asilia na Mbadala wako chini ya Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala ambalo mbali na majukumu mengine lina jukumu la kusajili watabibu wote wenye sifa zinazotakiwa baada ya kuwafanyia usaili. Lakini pia kuendeleza na kuboresha huduma hiyo.
Moja ya mikakati ya Baraza hilo kwasasa ni kuhakikisha kuhakikisha kuwa watabibu wote wa Tiba Asili wanapata usajili, ili kudhibiti vitendo vinavyotishia maisha ya binadamu ambavyo vimekuwa vikihusishwa na Tiba Asili.
Baraza linakiri kuwa ni kweli kuwa kuna idadi kubwa ya watu anbao wanajihusisha na huduma ya tiba asili kinyemela, kitu ambacho ni kinyume na sheria. 
Katika semina ya vyombo vya habari iliyoandaliwa na ATME jijini Dar es Salaam Mei 15 mwaka huu katika Ukumbi wa NMR Dar es Salaam,  Mlezi wa chama hicho, Kingunge Ngombale Mwiru alisema Watanzania wengi ni wazito  kukubaliana na Tiba Asili, hali ambayo alisema inachangiwa na dhana ya kutawaliwa na wakoloni.
Mwenyekiti wa ATME Simba Abdulhamani Simba anasema kuna umuhimu wa serikali kuhakikisha kuwa watabibu wote wa tiba asili wanasajiliwa ili kupunguza matukio ambayo yamekuwa yakifanywa na baadhi ya watu wanaojiita wataalamu  wa tiba, lakini kwa kuichanganya na vitendo vya kishirikina.
Boninventure Mwalongo ni Mkurugenzi wa Kliniki ya Tiba Asili ya Boresa ya jijini Dar es Salaam ambaye pia ni Mratibu wa ATME, anasema kuwa kwa sasa wako katika mkakati wa kuhakikisha wanawashirikisha wadau mbalimbali ili jamii itambue umuhimu

wa tiba asili, ikiwa ni pamoja na kutoa semina kwa wadau mbalimbali.

Mwalongo anasema kuwa jambo jingine ambalo linatakiwa kudhibitiwa ni matangazo holela ya waganga ambayo yamekuwa yakibadikwa na hata mengine kutumika katika vyombo vya habari bila kufuata utaratibu.
Aidha kumekuwa na uhusiano wa karibu kati ya wadau wa Tiba Asili na Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA). Mwaka 2012 kulikuwa na mkutano wa wadau wa dawa za asili. Halikadhalika Novemba 5 mwaka jana TFDA walikutana tena na wadau wa Tiba Asili.
Moja ya malengo ya mkutano huo ilikuwa ni pamoja na kukumbushana matakwa ya sheria pamoja na changamoto za udhibiti. Katika Mkutano huoMkurugenzi Mkuu waTFDA, Hiiti Sillo alisema kuwa moja ya changamoto katika Tiba Asili na Tiba Mbadala ni kuwepo katika soko bila kufuata taratibu za utengenezaji, lakini pia akasema akaongelea juu ya baadhi ya watu kutoa matangazo katika vyombo vya habari pasipo vibali vya Mamlaka hiyo.
Mwalongo anasema kuwa mikutano kama hiyo inadhihirisha jinsi Tiba Asili inavyozidi kupata uigo na kuzidi kuthaminiwa na kwamba watanzania wanapata mwanga zaidi wa kutambua kilicho bora na kuepuka udanganyifu kwa baadhi ya watu wanaojiita watabibu asili kinyume na utaratibu.
“Kwa ushirikiano kama huu nafikiri tutafika mahala watanzania walio wengi watafahamu umuhimu wa Tiba Asili kama ilivyo katika nchi za India na China ambako kwa mujibu wa takwimu za nchi hizo asilimia 80 za raia katika nchi hizo wanategemea Tiba Asili.
Ends.

Friday 5 September 2014

Utata kauli za Serikali ya kupiga marufuku matangazo ya tiba asili

  
masomo-bango-mganga
MABANGO ya matangazo ya waganga wa jadi yanaikoroga serikali kutokana na mara kadhaa kutoa maagizo ya kuyapiga marufuku bila mafanikio yoyote.
Taarifa zilizoifikia FikraPevu zimeeleza kwamba agizo hilo la mara kadhaa bila kutekelezwa kutokana na kauli hizo kutolewa bila ufuatiliaji katika kipindi cha miaka minne hadi sasa.
Aidha, licha ya serikali kutoa kauli hizo kupitia vyombo vya habari na Bunge, mabango ya wataalamu hao yanayojitangaza kutibu maradhi sugu yameelezwa kuwakera baadhi ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini kutokana na serikali kushindwa kutatua tatizo hilo.
Imebainika kuwa tangu tamko hilo kutolewa na serikali mwaka 2010 mabango hayo yameendelea kuwekwa zaidi katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, Tanga, Kigoma, Pwani, na mikoa ya kanda za juu kusini na kati bila serikali kuchukua hatua stahiki dhidi yao.
mmalawi-mganga-bango-kiboko
Matukio ya kishirikiana
Katika mtandao wa kuaminika wa kijamii wa JamiiForums kumekuwepo na mjadala wa matangazo hayo na kuwa mabango hayo hayalipiwi kodi licha ya wakati mwingine kuwekwa kwenye nguzo za umeme kinyume cha sheria.
mganga-freemason
Wamesema matukio ya mauaji yanayotokea katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo mkoa wa Mara na mikoa ya Kanda ya Ziwa, yanasababishwa na imani za kishirikiana kutokana na mabango hayo ambayo hueleza kutibu magonjwa sugu pamoja na kupandishwa cheo makazini na utajiri.
Utapeli kwa njia ya mabango
Mjadala huo umelalamikia hatua ya mabango hayo kuachwa yakijitangaza bila kulipa kodi.
“Sasa hivi Tanzania kuna staili mpya ya kupata fedha, huhitaji kutumia nguvu bali ni kucheza na akili ya mtu kwani kila unapopita utakuta tangazo la mganga wa kienyeji na wanaweka na namba za simu na kila mganga anaandika anatoka Sumbawanga, Tanga, Kigoma, au Pemba,” anaeleza mchangiaji mmoja wa JamiiForums.
DrMkombozi-cheo-kazini
Hata hivyo, wamesema mikoa ambayo imekithiri kwa zoezi hilo ni Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, Tanga, Kigoma, Pwani, na mikoa ya kanda za juu kusini na kati.
Kauli ya Serikali isiyotekelezeka
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, jana Jumanne Juni 3, 2014 alisema serikali imetangaza kuondolewa haraka mabango hayo kwa kile alichodai kuwa kuendelea kujitangaza kwa watu hao kutibu maradhi sugu ikiwemo Ukimwi, Shinikizo la damu na kisukari ni kosa kwa mujibu wa sheria.
Amesema Wizara hiyo, itatoa muongozo na taratibu zinazopaswa kufuatwa hivi karibuni, ili dawa husika ziweze kukaguliwa na kupimwa kitaalamu bila ya kutumiwa na wahusika.
Tafiti za waganga wa kienyeji
Hivi karibuni Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu NIMR, ilieleza kuanza mkakati utakaowezesha uhakiki wa dawa za waganga wa tiba asili nchini, ili kudhibiti viwango na afya za watumiaji.
Taarifa ya NIMRI ilisema hatua hiyo itawezesha kuhakikiwa kwa madawa ya waganga wa tiba mbadala ambao wamekuwa wakitoa huduma za kitabibu katika maeneo mbalimbali hapa nchini.  
Waganga wa tiba za jadi nchini, wamekuwa wakilalamikiwa mara kwa mara na wananchi wakiwataka kuacha kuwadanganya watu kuwa wanatibu magonjwa kama kifua kikuu, kisukari na Ukimwi kwa kuwa sheria haziwataki kujitangazana, licha ya baadhi yao kuendelea kutumia kutumia yiba hizo.
Kwa upande wa Kambi ya Upinzani Bungeni, imeitaka serikali kuwafutia vibali vya biashara, wafanyabiashara wanaoingiza vipodozi venye kemikali vilivyopigwa marufuku na mamlaka husika hapa nchini.
Wakichangia hotuba ya bajeti ya wizara hiyo, baadhi ya wabunge wamelalamikia hatua ya kitendo cha serikali kutoa asilimia 48 ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa mwaka wa fedha 2013/2014 licha ya umuhimu wa wiizara hiyo kubeba maisha ya Watanzania.

Ugonjwa wa Kisukari: Tafakari juu ya Chanzo, Dalili na tiba yake



Magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni magonjwa ambayo hayasambazwi kwa mtu mwingine kwa kuwa hakuna vimelea mwilini vinavyohusiana na magonjwa hayo. Magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni kama ya moyo na mishipa ya damu, figo, saratani, kifua sugu, kisukari, magonjwa ya akili na mengine ya kurithi kama vile ugonjwa wa selimundu (Sickle Cell Disease).
Ripoti ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) ya 2013, inadai magonjwa yasiyo ya kuambukiza ndio chanzo kikubwa cha vifo ulimwenguni, yakifanya asilimia 63 ya vifo vyote kwa mwaka. Magonjwa yasiyo ya kuambukiza huua watu zaidi ya milioni 36 kila mwaka. Asilimia 80 ya vifo vinasababishwa na magonjwa hayo hutokea nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi hizo. Inakisiwa kuwa mwaka 2020 magonjwa haya yasiyo ya kuambukiza yatasababisha asilimia 73 ya vifo vyote duniani na asilimia 60 ya ukubwa wa tatizo la magonjwa duniani.
Nchini Tanzania, katika mpango wa upimaji wa afya kwa magonjwa yasiyoambukiza jijini Dar es Salaam, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umebaini kuwa idadi kubwa ya wanaume wanapatwa na magonjwa hayo kuliko wanawake. Uchambuzi huo umeonyesha magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu na saratani zote ambazo zimekuwa chanzo cha vifo hivyo, huku serikali ikisema imeamua kuongeza juhudi za makusudi kupambana nayo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mfuko wa Bima ya Afya, athari ya magonjwa yasiyoambukiza ni mara nne zaidi ya watu waliopo mijini kuliko vijijini, huku asilimia 12.8 ya wanaougua wakiwa wako mijini na asilimia 3.1 wako vijijini kutokana na mfumo wa maisha.
Uchunguzi mwingine uliofanywa na jopo la madaktari bingwa kuanzia mwaka 2011 hadi 2014 ulibaini asilimia 79 ya watanzania wazee waligundulika kuugua magonjwa ya kisukari, macho na shinikizo la damu. Pia walidai magonjwa hayo yamekuwa kikwazo cha maendeleo kutokana na kuwasumbua wazee na hata wenye umri wa kati ya miaka 40 na 50.
Kisukari ikiwa ni moja ya muuaji wa kimya kimya katika kundi hili la magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Watu milioni 285 duniani kote wameathiriwa na kisukari ambayo ni sawa na asilimia 6.6 ya idadi ya watu wote ulimwenguni pia ikishika nafasi ya 5 kwa kusababisha vifo duniani.
Nchi zinazoongoza kwa idadi kubwa ya watu wenye kisukari ni China wagonjwa milioni 43.2, India wagonjwa milioni 40.9, Marekani wagonjwa milioni 25.8, Urusi wagonjwa milioni 9.6 na Brazil wagonjwa milioni 6. Nchi zenye idadi kubwa ya watu wazima wenye kisukari ni Nauru kwa asilimia 30, Bahrain kwa asilimia 25.5, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa asilimia 25, Saudi Arabia kwa asilimia 23.7 na Mauritius kwa asilimia 20.
KISUKARI NI NINI HASWA?
Sukari mwilini hutokana na vyakula pamoja na vinywaji tunavyotumia kila siku na hutumika kuupa mwili nguvu. Glukosi ni aina ya sukari ambayo huzipa chembe za mwili nishati. Hata hivyo ili glukosi iingie ndani ya chembe hizo inahitaji insulini. Insulini ni kemikali (Homoni) ambayo hutokezwa na kongosho (Pancrease).
Kisukari ni ugonjwa unaotokana na mtu kuwa na sukari nyingi kupita kiasi kwenye damu. Ugonjwa huo huvuruga utaratibu wa kuingiza sukari ndani ya chembe kutoka kwenye damu kwa kuwa chembe huhitaji sukari ili kupata nishati.
Ugonjwa wa Kisukari hutokea pale ambapo tezi ya kongosho inaposhindwa kutengeneza kichocheo (Homoni) aina ya insulin au pale mwili unaposhindwa kutumia vizuri kichocheo hicho na kusababisha kuongezeka kwa sukari (Hyperglycemia) au kushuka kwa kiwango cha sukari (Hypoglycemia). Ugonjwa wa kisukari unaweza kusababishwa na kuwa na kiwango kidogo cha insulin mwilini, mwili kutosikia kichocheo hicho au yote mawili.
TAKWIMU MBALIMBALI ZA UGONJWA  WA KISUKARI
Kulingana na ripoti mbalimbali karibu watu milioni 316 ulimwenguni pote wana kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu, ingawa wengi wao hawajui wana kiwango hicho. Kwa mfano, nchini Marekani pekee asilimia 90 ya watu wenye sukari nyingi kwenye damu hawatambui kama wana tatizo hilo. Ingawa asilimia 8.3 ya watu watu wa Marekani wana Kisukari ambayo ni sawa na watu milioni 25.8 na kufanya Kisukari cha 7 kusababisha vifo vya watu Marekani.
Mamilioni ya watu wana ugonjwa huo lakini hawana habari! Ni ngumu zaidi kutibu ugonjwa wa kisukari kwa kuwa mtu anaweza kuishi nao kwa muda mrefu kabla haujagunduliwa. Hiyo ndiyo sababu watu husema kwamba ugonjwa huo huua kimyakimya.
NINI CHANZO HASA CHA KISUKARI?
Ili kuelewa vyema ugonjwa wa kisukari ni muhimu kwanza kuelewa namna chakula kinavyovunjwa vunjwa na kutumiwa na mwili ili kuzalisha nguvu. Wakati chakula kinapoyeyushwa matukio kadhaa hutokea. Moja ni sukari inayoitwa glucosi ambayo ni chanzo cha nishati/nguvu mwilini huingia katika damu. Tukio la pili ni kiungo kinachoitwa kongosho (Pancrease) kutengeneza kichocheo cha insulini. Kazi ya insulini ni kuondoa glucosi katika damu na kuingiza katika misuli, seli za mafuta na ini, ambako hutumika kama nishati.
Watu wenye kisukari huwa na kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu kuliko inavyotakiwa kwa sababu miili yao haiwezi kupeleka sukari kwenye seli za mafuta, ini na misuli ili ihifadhiwe kwa ajili ya kuzalisha nguvu. Hii ni kutokana na moja ya sababu zifuatazo, huenda kongosho zao haziwezi kutengeneza insulini ya kutosha au seli za mwili wao haziathiriwi na insini kama inavyotakiwa au sababu zote hizo mbili.
Main Symptoms of Diabetes FikraPevu.com
Kama wewe ni mnene kupita kiasi, hufanyi mazoezi kwa ukawaida au una watu wa ukoo walio na kisukari, huenda tayari una kiwango cha juu cha sukari kwenye damu. Ongezeko la sukari kwenye damu mbali na kuwa kisababishi cha kisukari, hali hiyo inahusianishwa na hatari ya kupatwa na ugonjwa wa akili uitwao 'DEMENTIA'.
Kula sukari nyingi sio sababu ya ugonjwa wa kisukari. Lakini lazima tuseme kwamba kula sukari nyingi si nzuri kwa afya yako kwani utaongeza uzito wa kuweza kuathiri uwezo wa mwili wako kujikinga na maradhi tofauti. Ugonjwa wa kisukari umeitwa kwa kufaa "ugonjwa unaoathiri kiini cha nishati ya mwili". Mwili unaposhindwa kutumia glukosi, mifumo mbalimbali ya mwili inaweza kuacha kufanya kazi au hata kusababisha kifo.
Ugonjwa wa Kisukari kitaalamu hujulikana kama 'DIABETES MELLITUS'. Jina 'Diabetes Mellitus' linatokana na neno la Kigiriki linalomaanisha 'kunyonya' na neno la Kilatini linalomaanisha 'tamu kama asali'. Maneno hayo yanafafanua vizuri sana ugonjwa huo, kwani maji hupita mwilini mwa mtu aliye na ugonjwa wa kisukari kana kwamba yananyonywa na mdomo na kupitia kwenye njia ya mkojo kisha kutoka nje ya mwili. Isitoshe mkojo huwa na ladha tamu kwa kuwa una sukari. Ndiyo sababu kabla ya kuvumbua njia bora za kupima ugonjwa huo, mbinu moja ya kutambua kama mtu ana ugonjwa wa kisukari ilikuwa kumwaga mkojo wa mgonjwa karibu na kichuguu cha sisimizi. Ikiwa sisimizi wangevutiwa na mkojo huo basi hilo lilimaanisha kwamba mkojo una sukari.
NI NANI ANAWEZA KUWA NA UGONJWA WA KISUKARI?
Watu walio katika makundi yafuatayo wana uwezekano mkubwa wa kupata ugonjwa wa kisukari:-
– Wenye uzito uliozidi,
– Wenye historia ya kuwa na wagonjwa wa kisukari katika familia zao,
– Wanawake waliozaa watoto wenye kilo 4 au zaidi,
– Watu wasiojishughirisha au wasiofanya mazoezi,
– Wenye shinikizo la damu,
– Wenye msongo wa mawazo na
– Wenye matumizi makubwa ya pombe na sigara.
Watu hawa wanashauriwa kupima sukari yao kila mwaka wakiwa na umri wa miaka 45 na kuendelea.
Kuna hatari kubwa ya kuugua ugonjwa huo ikiwa mtu ana mafuta mengi katika tumbo na kiuno chake kuliko katika mapaja yake. Mafuta katika kongosho na ini huvuruga uwezo wa mwili wa kudhibiti kiasi cha sukari kwenye damu.
Wavutaji wa sigara wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi kwani zoea hilo hudhuru moyo na mfumo wa mzunguko wa damu na kubana mishipa ya damu. Kitabu kimoja kinasema kwamba asilimia 95 ya watu wanaougua kisukari ambao hulazimika kukatwa viungo ni wavutaji wa sigara.
DALILI ZA UGONJWA WA KISUKARI
~ Kunywa maji mengi kuliko kawaida na kusikia kiu kila wakati.
~ Kwenda haja ndogo mara kwa mara. Watoto kukojoa kitandani.
~ Kuwa dhaifu, kukosa nguvu na kujisikia mchovu kila wakati.
~ Kupungua uzito au kukonda licha ya kula vizuri.
~ Kusikia njaa kila wakati na kula sana.
~ Wanawake kuwashwa ukeni.
~ Kutoona vizuri.
~ Kupungua nguvu za kiume au hamu ya kujamiiana kwa wanawake.
~ Ganzi, kuchomwachomwa au kutohisi unapoguswa sehemu za miguu, viganja na vidole.
~ Miguu kuoza na hata kupata gangrini.
~ Kukaukwa na ngozi na pia kupata aina ya ngazi katika miguu.
~ Vidonda au majeraha sehemu yoyote ya mwili kutopona haraka.
~ Majipu mwilini.
Wenye dalili hizi wanashauriwa kupima sukari ili kubaini kama wana kisukari.

MWENYEKITI WA TRAMEPRO BWANA SIMBA ABDULRAHMAN SIMBA AKITOA SALAM ZA PONGEZI KWA MHE. DKT JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI KWA KUCHAGULIWA KUWA RAISI WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SEND EMAIL TO TRAMEPRO

Name

Email *

Message *