-

.

.

TRAMEPRO

TRAMEPRO

NAIPENDA NCHI YANGU TANZANIA

Friday 22 August 2014

CCM, UKAWA HAKUNA MBABE’

Viongozi wa Chama cha ukawa wakijadili jambo.
Na mwandishi wetu.
SAKATA la kuendelea au kutoendelea kwa Bunge Maalum la Katiba linalofanya vikao vyake mjini Dodoma, limeelezwa kuwa halitakuwa na mshindi endapo hakutakuwa na maridhiano baina ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Ijumaa limeambiwa.
Wakihojiwa kwa nyakati tofauti kufuatia kauli ya Katibu wa Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kudai kuwa chama chao kimebariki mchakato kuendelea, baadhi ya wananchi wamesema msimamo huo una faida na hasara zake kwa vile kinachotafutwa, si masilahi ya makundi hayo mawili pekee.
“Kuna mambo mengi sana ya msingi kwa Watanzania yanayotakiwa kujadiliwa katika katiba kuliko vitu vidogo vinavyowagawa hawa waheshimiwa, sasa hapa kunatakiwa maridhiano ya dhati ili katiba itakayopatikana isiwe na makengeza,” alisema Mwarami Jones, wa Dodoma, alipotoa maoni yake kwa njia ya simu.
Darren Pusa, msomi wa sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, alisema kisheria mchakato unaoendelea mjini Dodoma ni halali kwa vile kila kitu kipo kwa mujibu wa sheria, lakini kitakachotia doa ni katiba hiyo kuonekana kuandikwa na chama kimoja ambacho ni tawala.
“Inapoonekana kwamba CCM ndiyo inayoandika katiba, hiyo ni dosari, hata kama kuna vyama vidogovidogo vilivyobaki bungeni. Tatizo hapa kila mmoja anataka kuonyesha ana nguvu, mwisho wa siku Watanzania ndiyo wanaumia, vita hii haina mbabe,” alisema na kuziomba pande hizo mbili kufikiria kukaa mezani.
Jumanne na Jumatano Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi ilikutana mjini Dodoma kuzungumzia maendeleo ya mchakato wa katiba, wakati huu Ukawa ikiwa imesisitiza kuwa haitarejea bungeni kama Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Jaji Warioba haitajadiliwa.

RAIS KIKWETE AFUNGUA KITUO CHA AFYA KIBAONI, MOROGORO VIJIJINI‏

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akikata utepe kuashiria kufungua kituo cha Afya cha Kibaoni Morogoro vijijini Agosti 22, 2014.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Mama Salma Kikwete pamoja na Wabunge Mhe Abdul Mketeme (kushoto) na Mhe Getrude Rwakatale (kulia) wakifunua pazia kwa pamoja kuashiria kufungua kituo cha Afya cha Kibaoni Morogoro vijijini Agosti 22, 2014.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akikagua wodi mpya ya  kituo cha Afya cha Kibaoni Morogoro vijijini Agosti 22, 2014.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akitembezwa maeneo mbali mbali ya kituo cha Afya cha Kibaoni Morogoro vijijini baada ya kukifungua Agosti 22, 2014.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na wazazi baada ya kufungua kituo cha Afya cha Kibaoni Morogoro vijijini Agosti 22, 2014.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa  kituo cha Afya cha Kibaoni Morogoro vijijini Agosti 22, 2014.
PICHA NA IKULU

Tuesday 19 August 2014

Taarifa MPYA ya Wizara ya Afya kuhusu ugonjwa wa Ebola kuingia Tanzania.


Ugonjwa wa Ebola ambao kwa sasa umeingia kwenye headlines za dunia kutokana na kuripotiwa kwenye nchi mbalimbali za Afrika sasa umeingia kugusa vichwa vya habari na kuihusisha Tanzania.
 
 Waziri wa Afya wa Seif Rashid amesema wagonjwawaliohisiwa kupata maambukizo hayo kutokana na dalili za awali ni kutoka Benin na Mtanzania lakini baada ya vipimo wameonekana hawana maambukizo hayo.
 
Waziri Seif Rashid amesema kuwa tayari eneo maalumu limetengwa kwa ajili ya kufanyia uchunguzi wagonjwa wanaotiliwa shaka kuwa na ugonjwa huo ikiwa ni kauli iliyotoka baada ya kufanyiwa uchunguzi kwa wagonjwa wawili waliohisiwa.
ebola
 
Kupitia ukurasa wake wa facebook, Waziri Seif amesema vifaa maalumu vitakavyotumiwa na watoa huduma katika kuhudumia wagonjwa vimewekwa pia huku wizara ya afya ikiongeza uwezo wa kufanya uchunguzi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere ambao wasafiri wengi kutoka nje huutumia.

MGONJWA WA EBOLA' ASABABISHA TAFRANI SHINYANGA

Wakazi wa Manispaa ya Shinyanga, kwa siku mbili mfululizo walikumbwa na kiwewe, baada ya kuenea uvumi kwamba kuna mgonjwa wa mwenye homa hatari ya ebola, aliyefikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga. 

Taarifa za kuwepo kwa mgonjwa huyo, zilidai kuwa mgonjwa huyo alitoka katika moja ya mitaa ya Manispaa ya Shinyanga na  alikuwa akitokwa damu puani na mdomoni kabla ya kuzimia.
Akizungumzia hali hiyo jana, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk Ntuli Kapologwe alisema mgonjwa huyo ambaye alikuwa akitokwa damu mdomoni na puani, alifika hospitalini hapo juzi na baada ya kufika wauguzi na madaktari walitaharuki.
Kwa mujibu wa Dk Kapologwe, mgonjwa huyo alipelekwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), huku baadhi ya wauguzi na madaktari wakimkimbia hali iliyotia hofu kwa baadhi ya wahudumu na hata wagonjwa hospitalini hapo.
Hata hivyo, Dk Kapologwe alisema baada ya uchunguzi wa awali, ilibainika kuwa mgonjwa huyo ana matatizo ya kutokwa damu mara kwa mara na hajaambukizwa virusi hao wa ebola.
Akielezea namna mkoa ulivyojiandaa kukabiliana na ugonjwa huo uliokwishaua zaidi ya watu 1,000 katika nchi za Afrika Magharibi, Dk Kapologwe alisema waganga wakuu katika halmashauri zote sita za wilaya mkoani Shinyanga, wameshajiandaa.
Alisema wamekubaliana atakapogundulika mtu mwenye dalili za ugonjwa huo, taarifa itolewe mara moja katika ngazi ya mkoa, ambako kuna timu maalumu ya wataalamu iliyoandaliwa kushughulika na ugonjwa huo hatari.
Baada ya taarifa kutolewa kwa mujibu wa Dk Kapologwe, timu hiyo itathibitisha kama mgojwa ana dalili zote za ebola na taarifa kutolewa kwa umma.
Wakati ugonjwa huo ukisababisha kiwewe mkoani Shinyanga,   mkoani Kagera, Mkuu wa Mkoa, Fabian Massawe ameshauri wakazi wa mkoa huo kuwa macho na tayari kutoa taarifa kwenye vituo vya afya vilivyo jirani waonapo mtu mwenye dalili  za ugonjwa huo.
Alitoa mwito huo kupitia kwa waandishi wa habari aliozungumza nao jana ofisini kwake mjini hapa, baada ya kuibuka taarifa kuwa Rwanda kulikuwa na mtu anayehisiwa kuwa na ebola.
Hata hivyo, Waziri wa Afya wa Rwanda, Agnes Binagwaho alisema juzi kuwa mwanafunzi mmoja wa Ujerumani aliyefika nchini humo akitokea Liberia,  alihisiwa kuwa na ugonjwa huo lakini baada ya sampuli ya damu yake kupimwa katika maabara za kimataifa, hakukutwa na ugonjwa huo.
Massawe alisema Mkoa wa Kagera unapakana na nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na pia upo mwingiliano wa watu na shughuli mbalimbali za kijamii.
Alisema nchi jirani zikipata mlipuko wa ugonjwa huo, upo uwezekano wa kuvuka mipaka na kuingia mkoani Kagera, hivyo ni  wajibu wa kila mmoja kutoa taarifa akiona mtu anayedhaniwa kuwa na ugonjwa huo.
Dalili za ugonjwa huo unaoenezwa na virusi vya ebola ni pamoja na  kutokwa na damu sehemu mbali mbali za mwili, kuumwa na kichwa, mwili kuishiwa nguvu, maumivu ya misuli na hatimaye kifo.
Ugonjwa huo unaambukizwa kwa kugusa damu na majimaji ya mgonjwa pamoja na kugusa vifaa au nguo za mgonjwa.
Massawe alisema Kagera wamechukua hatua kwa kuweka mikakati kuhakikisha mlipuko wa ugonjwa  hauingii nchini  kupitia mipakani.
Miongoni mwa halmashauri ambazo zimeelekezwa kuchukua hadhari kutokana na kuwa mpakani mwa nchi, ni wilaya ya Bukoba, Missenyi, Karagwe, Kyerwa

DK. MWINYI ATAKA WAGANGA WA TIBA ASILI KUSHIRIKIANA NA WATAFITI

a5d0Dr-Hussein-Mwinyi


                                            Dk. Hussein Mwinyi

NA MAGRETH   KINABO – MAELEZO

WAZIRI wa Afya na  Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi amewataka  waganga  wa tiba asili washirikiane na wataalamu wa utafiti ili kuwezesha upatikanaji wa dawa bora na salama.

 Kauli hiyo ilitolewa leo na Waziri huyo wakati akitoa tamko kuhusu maadhimisho ya siku ya tiba ya asili ya mwafrika ambayo huadhimishwa kila mwaka Agosti 31, lakini mwaka huu hayakufanyika kutokana na uhaba wa fedha. Maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika mwakani kipindi  katika hicho.

“ Tanzania tunayo mitidawa mingi na mingi haijafanyiwa kazi katika utafit na kuweza kubaini uwezo wa kutibu magonjwa mbailmbali tatizo lililopo ni jinsi gani mitidawa hiyo inweza kufanyiwa utafiti na kuwa dawa bora na salama kwa watumiaji kwa kuziwekea mifumo ya huduma za afya ili kila mwenye kuhitaji aweze kuzipata,” alisema Dk. Mwinyi .

 Dk. Mwinyi aliwataka waganga hao kushirikiana na watafiti kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR)  na  Taasisi  ya  Utafiti wa Dawa za Asili iliyokpo katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi  Shiriki- (MUHAS).

 Aliongeza kuwa waganga wote wa tiba asili na tiba ya kisasa wanatakiwa kufanya kazi kwa kuelewana ili kuwezesha kupata taarifa za awali kabla ya utafiti kamili kufanyika.

 Aliitaja kauli mbiu ya maadhimisho hayo kuwa ni ‘ Tiba Asili : Utafiti na Maendeleo’ kuwa inalenga kutoa majukumu  kwa waganaga wa tiba asili na tiba mbadala katika sula zima la utafiti. Pili inatoa changamoto juu ya uendelezaji wa taarifa za utafiti wa mitidawa katika kutafuta dawa ya kutibu magonjwa mbalimbali.

 Aidha aliwahimiza waganga wa tiba asili kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao na huduma za afya.

Wednesday 13 August 2014

TAZAMA PICHA_ MTANGAZAJI WA CLOUDS FM KIBONDE AKISHIKISHWA ADABU NA ASKARI WA USALAMA BARABARANI LEO JIJINI DAR ES SALAAM..KUHUSU MTANGAZAJI KIBONDE WA CLOUDS FM KUSABABISHA AJALI KISHA KUDAKWA JUU JUU NA ASKARI AKITOROKA


 

Mtangazaji Mahiri wa Redio Clouds FM Ephrahim Kibonde akidhibitiwa na

 Askari wa Usalama barabarani.

Mtangazaji Mahiri wa Redio 88.5 Clouds FM kupitia kipindi cha Jahazi, Ephrahim Kibonde amedhibitiwa na Askari wa Usalama barabarani wakati alipotakiwa kutii sheria bila shurti,mapema leo asubuhi jijini Dar es salaam.



Kibonde anadaiwa kusababisha ajali asubuhi ya leo eneo la Makumbusho, ikiwa gari aliyokuwa akiendesha kuigonga gari ya dereva mwingine kwa nyuma. 

Trafiki walifika eneo la tukio na kupima ajali, Kibonde alipoona hivyo akarudi nyuma na kuendesha gari lake kuondoka eneo la tukio bila kufuata taratibu za usalama barabarani,hali iliyomlazimu yule Trafiki kutumia gari lililogongwa kumfukuzia. 

Walifanikiwa kumkamata eneo la Mwenge na Trafiki aliingia katika gari lake na kumwomba arudi eneo la ajali ili wakapime na kuchora mchoro wa ajali. Kibonde aligoma na kumtaka trafiki ashuke katika gari lake,Trafiki naye hakutana kufanyi kwa maana ya kuwa aligoma kushuka na kumuamuru Kibonde arudi eneo la tukio.



Kibonde aliondoa gari na kuendelea na safari yake huku yule Trafiki akiwa ndani ya gari hiyo, Trafiki aliwasiliana na wenzake ambao walianza kuifuatilia gari hiyo ya Kibonde kama walivyopewa maelekezo na mwenzao aliopo ndani ya Gari hiyo.



Mara Kibonde akatokea maeneo ya mataa ya Ubungo, hapo kulikuwa na Trafiki mwingine aliyekua eneo hilo akaipiga mkono gari ya Kibonde na ambapo inasemekekana hakusimama na badala yake ikaja gari nyingine na kuichomekea kwa mbele na hapo ndipo alipotiwa mbaroni!



Aligoma kuendesha gari ikabidi livutwe hadi polisi Urafiki na yeye kuwekwa chini ya ulinzi na baadae akahamishiwa Kituo cha Oystabay ambako yupo mpaka sasa.

Inadaiwa kuwa Kibonde alikuwa amelewa sana,hali iliyopelekea kufanya hayo yote ikiwa ni pamoja na kuwajibu vibaya Askari hao.



Makubwa yasiyo na saizi_ TAZAMA PICHA ZA JAMAA ANAYEDAIWA KUMPA MIMBA MBWA HUKO DAR ES SALAAM


Bw. Hamis Juma akijitetea kuhusiana na shutuma za mkewe.
  “Na tangu mume 
wangu aanze mchezo huo huyo mbwa mmoja mweusi (pichani) amenawiri kupita kiasi, naamini amempa mimba.


Kweli dunia sasa ni vululuvululu! Mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Cecilia Hamis (pichani), mkazi wa Majoe Mjimpya Relini jijini Dar es Salaam amemlalamikia mumewe aliyemtaja kwa jina la Hamis Juma kwamba ametembea na mbwa wao mweusi hadi kumpa mimba.Akizungumza na Uwazi mwishoni mwa wiki iliyopita nyumbani kwake, mwanamke huyo alisema alibaini hilo wiki mbili zilizopita.

Mwanamke  anayejitambulisha kwa jina la Cecilia Hamis akiwa na mume wake(mtuhumiwa) Hamis Juma.
 

 SIMULIZI YENYEWE
“Nililigundua hilo wiki mbili zilizopita. Nakumbuka ilikuwa usiku nikiwa nimelala, nikamsikia mbwa mmoja (kati ya wawili) analia. Niliamka kwenda kuangalia ili kujua sababu, kufika nikawasha tochi ya simu, nilishangaa sana kumwona mume wangu yuko naye amemshikilia (asomaye na afahamu).

“Nilimuuliza anachokifanya, akasema anammalizia shida zake kwa kuwa hakuna mbwa wa kiume wa kumsaidia,” alisema mwanamke huyo.
 MARA YA PILI
Akiendelea kumlalamikia mume wake kwa madai hayo mazito, mama huyo alisema:
“Siku iliyofuata usiku tena, nikiwa nimelala nilimsikia mbwa akilia, nikaamka. Safari hii niliambatana na watoto wangu, tukaenda nje, kufika tukamshuhudia mume wangu akifanya tukio kama la jana yake, nilipomuuliza akanipa majibu yaleyale kwamba anammaliza shida zake mbwa huyo.”
Akaendelea: “Hawa mbwa waliletwa wawili wakiwa wadogo kabisa na wote ni majike na tangu walipoletwa sijawahi kumwona mbwa dume hata siku moja kwani mara nyingi tunawafungia kwenye banda lao.
 
 AWAELEZA MAJIRANI
Mwanamke huyo alisema kutokana na kukithiri kwa tabia hiyo, aliamua kuwaeleza majirani ambao nao walimshauri aende kuripoti kwa mjumbe wa eneo hilo.
 MJUMBE MWENYEWE HUYU HAPA
Akizungumza na Uwazi, Mjumbe wa Shina Na. 26, Majoe Mjimpya, Mbaruka Nyamaishwa alikiri kupokea malalamiko hayo kutoka kwa mwanamke huyo akamshauri kuyapeleka kwenye Kituo cha Polisi cha Stakishari.
Mbwa anayedaiwa kupewa mimba na Bw. Hamis Juma.
 MAJIRANI WAONA ANACHELEWA
Habari zaidi zinawekwa wazi kwamba, majirani nao walipoona mwanamke huyo anachelewa kwenda polisi, wao walimsomba na kwenda naye ambapo walitoa taarifa katika Dawati la Jinsia.
Mkuu wa dawati hilo, Koplo Golbert aliongozana na walalamikaji hao hadi nyumbani kwa mdaiwa ambapo alimkagua mbwa huyo na kuwaamuru wanandoa hao kuripoti kwenye kituo hicho cha polisi bila kukosa jana Jumatatu saa 3 kuonana na mkuu huyo na uchunguzi kuendelea.
 SWALI LA MSINGI
Uwazi lilimuuliza swali moja mwanamke huyo, ni kwa nini anasema aliamka na kutoka nje usiku bila kueleza mumewe anakuwa wapi muda huo kwani hakuonyesha kushangaa kutomwona kitandani?
Anajibu: “Tulitengana vyumba kwa sababu ya ugomvi wa kifamilia.”
Mbwa huyo akicheza na mwenzie.
 JE, MUME ANASEMAJE?
Uwazi lilimgeukia mume wa mwanamke huyo na kumuuliza kuhusu madai mazito ya mkewe ambapo alisema:
 “Mimi sijawahi kufanya kitendo hicho na mbwa ila nahisi mke wangu na hawa majirani wa hapa wananitengenezea hilo tukio ili nikafungwe jela maisha, halafu wao waweze kuchukuwa mashamba yangu kwani ndani ya ndoa yangu kumekuwa na ugomvi wa mara kwa mara.”
 UWAZI LAMUULIZA DAKTARI WA MUHIMBILI
Uwazi lilitilia shaka uwezekano wa mbwa kunasa mimba ya binadamu, hivyo lilimsaka daktari mmoja wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kumuuliza kuhusu madai ya mwanamke huyo.
Msikie: “Mh! Binadamu kumpa mimba mbwa haiwezekani. Binadamu anaweza kumpa mimba sokwe, kwa mbali sana nyani. Lakini si mbwa.
 “Ila kama huyo mama anasema hivyo, mbwa akapimwe na ikibainika ni kweli basi yatakuwa maajabu ya dunia maana dunia ina mambo yake.”

MWANAMKE MWENYE UJAUZITO WA MIEZI 9 AOGELEA KWA KUTUMIA MABOGA KUVUKA MTO KWENDA KUJIFUNGUA HOSPITALINI


Mwanamke mmoja nchini India ameogelea kwenye mto uliokuwa umejaa maji mengi yaliyotokana na mvua kubwa ilhali akiwa na ujauzito wa miezi tisa.

Anasema sababu ya safari yake majini ni ili aweze kufika katika kituo cha afya aweze kujifungulia hospitalini.

Mama huyo kwa jina Yellawa alitumia maboga makavu yenye maganda magumu yaliyomsaidia kuogelea kwa umbali wa karibu kilomita moja kutoka kwenye kijiji chake kusini mwa jimbo la Karnataka.

Alishikwa na uoga lakini alitaka kujifungua salama, hakuna kituo cha afya kijijini kwake na hakutaka kujifungulia nyumbani.
Wanakijiji na madaktari wamesifu hatua yake ya kuogelea kuwa ni mafanikio makubwa.
Yellawa ni binti wa miaka 22, kutoka kijiji cha Neelakantarayanagadde, kijiji kidogo kando kando ya mto Krishba kaskazini mwa mji wa Bangalore.
Namna pekee ya kusafiri kutoka katika kijiji hicho kwa kuvuka mto ni kwa kutumia miti iliyotengenezwa kwa kuunganishwa mithili ya boti, kifaa ambacho hata hivyo si imara na hakifanyi kazi nyakati ambazo mto huwa umejaa maji.
Wakati Yellawa akiogelea kuvuka mto juma lililopita, maji yalikua yameongezeka ambapo alishuhudia waogeleaji wakisita kuingia kwenye maji.
Binti huyu alishikwa na hofu lakini alijipa moyo kuwa anafanya vile kwa usalama wa mtoto wake.
Yellawa alisaidiwa na baba yake, kaka na ndugu zake ambao waliogelea pamoja naye.
Ingawa alikua amechoka lakini daktari aliyekuwa akimchunguza alipowasili katika hospitali ya serikali karibu na kijiji cha Kekkera alisema kuwa anaendelea vizuri na yuko nyumbani kwa nduguye amepumzika.

Yellawa anasifiwa kwa ushujaa wake wa kuvuka mto kwa hali ya ujauzito aliokuwa nao

MGANGA WA JADI ADAIWA KUMKATA MKONO ALIBINO HUYU AKIWA NA WENZAKE KISHA KUTOKOMEA KUSIKOJULIKANA NA MKONO HUO

MGANGA WA JADI ADAIWA KUMKATA MKONO ALIBINO HUYU AKIWA NA WENZAKE KISHA KUTOKOMEA KUSIKOJULIKANA NA MKONO HUO


Ukatili dhidi ya wenye ulemavu wa ngozi (Albino) umejitokeza tena mkoani Tabora ambapo mtoto Pendo Sengerema (14) mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi Nundu, amekatwa mkono wake wa kulia na wahalifu kukimbia nao kusikojulikana na aliyeshiriki uharifu huo akihaidiwa kulipwa laki tisa huko katika kijiji cha Usinge wilayani Kaliua.

Akiongea kwa tabu alipolazwa katika hospitali ya wilaya ya Urambo mkoani Tabora majeruhi Pendo Sengerema amesema kuwa, aliyemkata mkono alimfahamu maana ni jirani anayesadikiwa kuwa, ni mganga wa kienyeji, ambapo kaimu mganga wa hospitali hiyo, Dokta James Kang’oma, akidai kuwa walijitahidi kuokoa maisha yake kutokanana kutoka kuvuja damu nyingi.

Mratibu wa chama cha wenye ulemavu wa ngozi wilaya za Urambo na Kaliua Bw Focus Mgesera, amesema kuwa, pamoja na mtoto huyo kulazwa katika hospitali hiyo bado kuna hali ya hatali kwake kwani kwa namna moja ama nyingine anaweza kuuawa kutokana na kuwafahamu waliomjeruhi, hivyo anahitaji ulinzi.

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Under the same sun, Bi Vicky Ntetemya aliyefika hospitalini hapo kumwona mtoto huyo amesema kuwa, serikali iwe makini na jamii ya wenye ulemavu wa ngozi kutokana na masuala ya wagombea nafasi za uongozi kujishirikisha ma mambo ya waganga wa kienyeji.

Chama cha walemavu wa ngozi nchini kimeraani tukio hilo kikitaka serikali kuongeza ulinzi kwa jamii hiyo ambapo akizungumza kwa njia ya simu, kamanda wa polisi mkoani Tabora Suzan Kaganda akidhibitisha kutokeaa tukio hilo.

HII HAPA HOTUBA YA MWENYEKITI WA BUNGE MAALUM LA KATIBA MHE. SAMUEL SITTA KATIKA UFUNGUZI WA AWAMU YA PILI YA BUNGE HILO, DODOMA AGOSTI 5,2014

HII HAPA HOTUBA YA MWENYEKITI WA BUNGE MAALUM LA KATIBA MHE. SAMUEL SITTA KATIKA UFUNGUZI WA AWAMU YA PILI YA BUNGE HILO, DODOMA AGOSTI 5,2014

Karibuni tena Dodoma Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la kutunga Katiba ya nchi yetu. Sote tuna kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu wetu kwa kuendelea kutupa uhai na afya hadi leo kutuwezesha kuwepo ndani ya ukumbi huu. Tupo humu ili tuitekeleze kazi waliyotukabidhi Watanzania wenzetu milioni arobaini na sita (46) ya kuwapatia Katiba mpya. Dhamana hii ni nzito na haistahili kufanyiwa ajizi.

Tunaendelea na shughuli zetu za Bunge Maalum kwa kuzingatia Kanuni ya 30 (1) inayosema
Akidi kwa kila kikao cha Bunge Maalum isipokuwa wakati wa kupitisha uamuzi wa Bunge Maalum itakuwa ni nusu ya Wajumbe wote wa Bunge Maalum“.
Nimetaarifiwa na Katibu kwamba wajumbe waliokuja Dodoma kuhudhuria ni zaidi ya robo tatu ya Wajumbe wote wa Bunge Maalum. Nawashukuruni nyote kwa kuja hapa Dodoma ili kutimiza wajibu wenu.
Kwa niaba yenu, nawashukuru Watanzania wenzetu wote ambao kwa mamilioni wamedhihirisha utashi mwema wa kisiasa kwa kuunga mkono hatua ya Bunge Maalum kuendelea na kazi zake hadi tuipate Katiba inayopendekezwa ambayo wataipigia kura ya maoni. Kipekee na kwa niaba yenu, nawashukuru kwa dhati viongozi wetu wa dini wa madhehebu yote wanaloliombea Taifa hili mafanikio Bunge Maalum, wakitanguliza utaifa pamoja na amani ya nchi na umoja ndani ya nchi na siyo ubinafsi na maslahi ya makundi.
 Kwa leo sikupenda sana kuzungumzia hoja mbali mbali zinazotawala magumzo ya mchakato wa Katiba mpya hapa nchini, magumzo yanayoendeshwa na makundi maalum kwa jazba na hata matusi. Hata hivyo nalazimika kutoa maelezo ya ufafanuzi kuhusu upotoshaji mkubwa unaoendeshwa na baadhi ya watu kuhusu Bunge Maalum. Nikiwa Mwenyekiti wenu ninao wajibu wa kuwafafanulia wananchi kuhusu uhalali wa shughuli za Bunge Maalum linaloendelea na utaratibu wa shughuli zetu.
Ni Rasimu ya Tume au la
Wapo wanaodai kuwa eti hapa Bungeni hatujadili Rasimu ya Tume. Tuhuma hii haina ukweli hata kidogo. Msingi wa majadiliano yote tangu tumeanza ni Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Katiba. Utaratibu ni kwamba pale ambapo wajumbe wanaona panafaa kurekebishwa wanafanya hivyo. Maana ya rasimu ni andiko ambalo halijajitosheleza bila kupata ithibati ya taasisi ya juu zaidi. Anayekabidhiwa rasimu anayo haki na mamlaka ya kuirekebisha. Vinginevyo kujadili rasimu hakuna sababu. Itakuwa ni jambo la ajabu na lisilo na mantiki yoyote kuwa taasisi iliyopewa mamlaka ya kujadili Rasimu ikishaijadili iiache ibaki kama ilivyokuwa wakati ilipowasilishwa!
 Je suala ni muundo wa Muungano tu?
Maudhui ya Rasimu yanajumuisha baadhi ya masuala muhimu yafuatayo:
-      Kuimarisha Muungano wetu kwa kuleta uwiano     bora zaidi wa mamlaka ya Zanzibar na Tanzania      Bara ndani ya Muungano
-      Kuimarisha haki za binadamu ili kuwawezesha      raia wa kawaida kufaidi uhuru wa demokrasia     bila ubabe na dhuluma
-      Kuzuia wachache kufuja rasilimali za taifa bila       kujali maslahi ya wengi na ya vizazi vijavyo.
-      Kujenga uwiano sahihi na wenye haki baina ya      wanawake na wanaume katika nafasi za uongozi.
-      Kubainisha hatua zenye kuleta matumaini mapya ya maendeleo kwa makundi maalum ya vijana     wakulima wadogo, wafugaji, wafanyakazi wa ngazi   za kawaida, walemavu, wafanya biashara wadogo   na wajasiriamali wengine.
-      Kuweka msingi imara wa kutungwa kwa sheria      kakamavu za kuzuia ukandamizaji wa raia,        unyonyaji, wizi wa mali ya umma, rushwa,    hujuma dhidi ya uchumi na kuzuia mapato        haramu na fedha chafu.
-      Kutambua haki za ardhi kwa wakulima, wafugaji    na wajasiriamali wengine ili kupunguza migongano na migogoro.
-      Kuweka Misingi ya utawala bora inayozingatia        uadilifu, sifa stahiki na ufanisi.
-      Kuwezesha kutungwa kwa sheria bora zaidi     zitakazosimamia chaguzi zilizo za haki na huru    zaidi pamoja na kuwepo Tume za Uchaguzi       zilizoboreshwa.
Zaidi ya hivyo, yapo mapungufu katika Rasimu iliyopo kwa kuachwa masuala ya kuwezesha Serikali za mitaa; kutoa maelekezo kuhusu masuala ya matumizi ya ardhi na rasilimali nyingine za Taifa. Nini kinatuzuia kuiboresha Rasimu kwa kuyaongeza mambo haya ndani ya Katiba kwa faida ya Taifa?
 Yote haya ni masuala muhimu ambayo yamo ndani ya rasimu na wakati wake wa kuyaweka sawa ndiyo huu. Pamoja na umuhimu wake suala la muundo wa Muungano si suala la kutulazimisha tuyaahirishe mazuri yote yaliyomo katika Rasimu tuliyopewa.
 Uhalali wa Shughuli za Bunge Maalum
Pamoja na uhalali wa kisheria wa Bunge hili Maalum kuendelea kufanya kazi zake, linao pia uhalali wa kisiasa kutokana na sifa za uwakilishi wetu na pia maudhui yaliyomo ndani ya Rasimu. Kutofautiana maoni hakuwapi hadhi tofauti baadhi ya wajumbe kujiona wao wana uhalali zaidi mbele ya wananchi kuliko wenzao. Ndiyo maana utaratibu umewekwa wa kupiga kura na wa maridhiano. Utamaduni mpya unaoanza kujengwa na baadhi ya viongozi wa jamii wa kususia mijadala halali na kwenda nje kuelezea hoja za upande mmoja hauna nafasi katika Tanzania jamii isiyotaka fujo na utengano.
 Wajumbe wa Bunge Maalum wanaoendelea na kazi mjini Dodoma ni wateule wa Rais kwa niaba ya wananchi kwa kazi ya kutunga Katiba. Kazi hii haiwezi kusitishwa kwa sababu tu wajumbe wachache wameisusia. Tutazingatia matakwa ya sheria katika kufikia hatma ya mchakato wa Katiba.
 Mabadiliko ya Kanuni
Kama nilivyoeleza hapo mwanzo, Rasimu ina jumla ya sura kumi na saba (17) zenye mambo mengi yenye maslahi kwa Watanzania wote. Kwa muda tuliopewa wa siku sitini (60) isingewezekana kuikamilisha kazi tuliyopewa ndani ya muda. Ikumbukwe kwamba kwa Kanuni zilivyo, kila sura mbili zinahitaji siku tisa kuzifanyia kazi. Kwa njia hiyo, ingetuchukua siku takriban mia moja thelathini (130) ili kuikamilisha kazi hii! Pendekezo la msingi hapa ni kwamba Kamati zetu kumi na mbili (12) zizingatie na kuzijadili sura kumi na tano (15) za Rasimu na pia zikamilishe uandishi wa sura mbili zilizojadiliwa awali na ikibidi ziongeze sura ambazo zitadhihirika kuwa ni muhimu. Naamini mtiririko huu utatuwezesha kuwa na mpangilio bora zaidi wa sura na ibara katika Katiba mpya. Tusingependa na wala isingefaa kuomba tena muda wa ziada wa kazi ya Katiba ndio maana tunafanya mabadiliko ya Kanuni. Kamati ya Uongozi iliyoketi Dar es Salaam tarehe 28 Julai 2014 imependekeza yafanywe mabadiliko ya Kanuni za Bunge Maalum kuwezesha kazi ikamilike ndani ya muda tuliopewa. Kwa hiyo nitawaomba tuyatafakari mapendekezo ya mabadiliko ya Kanuni na hatimaye kuyapitisha ili ratiba ya kazi zetu iende sawa. Nitawaomba muikubali ratiba iliyogawanywa leo na pia mkubali kuzibadilisha Kanuni kwa lengo nililolieleza hapa.
 HITIMISHO
Pamoja na maoni ya kila namna yanayoendelezwa kujadili mchakato wa Katiba nje ya Bunge hili, ni muhimu wahusika wapunguze jazba, chuki na upotoshaji. Bunge Maalum lisaidiwe kwa mawazo chanya ili limalize kazi yake.
Sisi tuliomo humu katika Bunge Maalum tuna wajibu wa kuifanya kazi yetu kwa umakini na kwa uadilifu ili kazi yetu iwe bora. Tujadiliane kwa uungwana. Tofauti za mawazo zisitufanye tuingize chuki na maneno yasiyofaa. Katika mabadiliko ya Kanuni nashukuru sasa Kiti kimepewa mamlaka ya kushughulikia utovu wa nidhamu ndani ya wakati. Lakini ninaamini haitakuwa lazima kwangu mimi au Makamu Mwenyekiti kutumia nguvu za mamlaka yetu ila tu pale itakapobidi.
 Nawatakia nyote Mkutano wenye mafanikio kwa maslahi mapana ya nchi yetu.
 MUNGU IBARIKI TANZANIA!
 Samuel Sitta – MB

MWENYEKITI BUNGE MAALUM LA KATIBA

MWENYEKITI WA TRAMEPRO BWANA SIMBA ABDULRAHMAN SIMBA AKITOA SALAM ZA PONGEZI KWA MHE. DKT JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI KWA KUCHAGULIWA KUWA RAISI WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SEND EMAIL TO TRAMEPRO

Name

Email *

Message *