-

.

.

TRAMEPRO

TRAMEPRO

NAIPENDA NCHI YANGU TANZANIA

Wednesday 27 April 2016

Madhara ya kuchanganya dawa za hospitali na za asili

Image result for panadol

Wakati mwingine mwingiliano kinzani wa kiutendaji wa dawa za asili na zile za hospitalini, unaweza kusababisha dawa kugeuka kuwa sumu na kusababisha mzio hatari wa kuzimia na kushindwa kupumua.
Watu wanaougua magonjwa sugu wamekuwa wakijikuta kwenye mkanganyo kiasi cha kuwafanya watumie dawa za hospitalini pamoja na zile za asili bila kujua athari mbaya zaidi zitakazowapata. Matumizi ya dawa za asili au tiba mbadala kwa sasa yameenea sana. Za asili zinajizolea umaarufu sehemu mbalimbali duniani kutokana na kupigiwa debe muda mwingi




Dawa za asili.
Sheria za kimataifa zinapiga marufuku dawa za hospitalini kutangazwa kwa sababu mwenye mamlaka ya kuamua matumizi ni daktari na wala si mgonjwa Dawa za hospitalini hadi ziidhinishwe kwa matumizi ni lazima zipitie hatua mbalimbali kuthibitisha viwango vya kutibu, faida na hasara. Dawa za asili zimekuwa zikitumika ama kutokana na mazoea au mgunduzi kuzitangaza wakati athari zake zinazotokana na kiwango cha sumu kilichopo kutokujulikana.Pamoja na hali hiyo, jambo la hatari zaidi ni watu wengi kuchanganya dawa hizi za asili na zile zinazotengenezwa maalumu kutolewa hospitalini.Wagonjwa wengi hasa wenye magonjwa sugu yanayoelekea kushindikana hospitalini wanatumia tiba za asili kubahatisha uwezekano wa kupona. Wengine kwa kutokujiamini hujikuta wanaenda hospitali kupata dawa na wakati huo huo huenda kwa waganga wa jadi kupata huduma.Wengine wanapokwenda kuonana na madaktari, huwa hawako tayari kuweka wazi kwamba wanatumia dawa nyingine za asili.Kuna baadhi ya waganga wa jadi, kwa tamaa zao huwa wanawaambia wateja wao kuwa dawa zao haziwezi kuingiliana na zile za hospitali kwa kuwa ni kama chakula tu.
Ukweli ni kwamba nyingi zina sumu.Taarifa nyingi za kitabibu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa wapo watu wengi wanaochanganya dawa hizi na kujikuta wanatengeneza tatizo jingine ambalo pengine ni kubwa zaidi ya lile linalowasibu.Katika utafiti huo, inaonekana kwamba madhara ya mwingiliano ama ukinzani wa dawa za asili na zile za kisasa, linaongezeka.Hata hivyo, taarifa hizi zinaweza kuwa hazitoi picha kamili kwa vile takribani asilimia 70 ya wagonjwa walioathirika, hawaelezi ukweli wa kuchanganya dawa.Kwa sababu hiyo hakuna utaratibu maalumu wa kuweka takwimu ili kufuatilia ukubwa wa tatizo hilo.
Dk Shufeng ZHOU aliandika makala kwenye jarida la ‘Herbal Medicine  Drug Interactions’ nchini Singapore, toleo la 6, akielezea juu ya utafiti wa matumizi mchanganyiko wa dawa za asili na zile za hospitalini.Dk Zhou anasema matumizi ya namna hiyo yanaweza kusababisha mwingiliano au ukinzani wa dawa na kusababisha madhara makubwa kwa mtumiaji.Matumizi ya namna hii yanaweza kuzuia dawa moja isifanye kazi, au moja iwe na nguvu zaidi kuliko kawaida na kudhuru mwili.Dawa zote zinaweza kujishikiza katika vipokeleo vya dawa vya aina moja na kushindana au kuzuia uzalishaji wa vimeng’enyo vya mwili visisafirishe dawa mwilini kama inavyotakiwa.Hali ya namna hii inaweza kusababisha usugu wa viini vya magonjwa hatari dhidi ya dawa mfano Viini vya Kifua Kikuu (TB), Virusi Vya Ukimwi (VVU), au kudhurika kwa ini na figo na kusababisha viungo hivi vya mwili, kushindwa kufanya kazi zake vizuri. Wakati mwingine mwingiliano kinzani wa kiutendaji wa dawa za asili na zile za hospitalini, unaweza kusababisha dawa kugeuka kuwa sumu na kusababisha mzio hatari wa kuzimia na kushindwa kupumua.Hatari ya mwingiliano kinzani wa utendaji wa dawa, huwa mkubwa zaidi pale dawa zaidi ya moja zinapotumiwa kwa pamoja.Mtafiti mmoja wa maswala ya dawa anasema kuwa, mtu anapotumia dawa mbili kwa wakati mmoja, hatari ya mwingiliano kinzani ni asilimia 6. Anapotumia aina tano za dawa mwingiliano ni asilimia 50 na hatari huongezeka zaidi hadi kufikia asilimia 100 pale mtu anapochanganya dawa nane au zaidi.
Hii ni kwa mujibu wa Kuhn Merrily, katika kitabu chake cha “Pharmacotherapeutics: A Nursing Process Approach. Philadelphia, Pa: FA Davis, 1998”.Dawa zinapoingiliana kiutendaji, hutengeneza mazingira yasiyofaa katika tumbo la chakula na utumbo, kiasi kwamba sehemu hizi za mwili hushindwa kufanya kazi ipasavyo. Matokeo yake ni kuharisha, kupata kichefuchefu au kupata vidonda vya tumbo au mwili kushindwa hufyonza kiasi cha kutosha cha dawa kwa ajili ya kupambana na ugonjwa. Mfano mzuri ni pale mtu anapotumia aloe vera na dawa za hospitalini kwa wakati mmoja anaweza kuharisha.
 Pia mwingiliano kinzani unaweza kusababisha dawa kujishikiza katika vipokeleo visivyo vya kawaida na kushindwa kusambaa kama inavyotarajiwa. Tatizo jingine hutokea wakati dawa zilizoingiliana kiutendaji zinapofika ndani ya ini. Hapo dawa huathiri vimeng’enywa vya ini vinavyoshughulikia dawa, vijulikanavyo kama CYP 450 enzymes na P-glycoprotein. Hali hii huweza kupunguza au kuongeza makali ya dawa kwa namna isiyokuwa ya kawaida.Hatari haiishii hapo, dawa zinapoingiliana kiutendaji pia huathiri utendaji wa figo na kushindwa kuondosha kiasi kikubwa cha sumu hatari mwilini. Hali hii inaweza kudhuru figo na kusababisha kiungo hicho muhimu kufa au kuwa dhaifu kiutendaji. Mwingiliano wa Dawa tunazotumia huathiri miili yetu kwa wema au kwa ubaya. Dawa zinapoingiliana kiutendaji zinaweza kupingana au kuongezeana nguvu na kuleta ufanisi au kuongeza makali ya dawa na kuwa sumu.  Baadhi ya dawa za asili zitokanazo na mimea huongeza makali ya dawa za hospitalini na nyingine hupunguza makali yake na kuvuruga kazi iliyokusudiwa ya kupambana na vimelea vya magonjwa Dawa za hospitalini pia huweza kuingiliana na zile za kufukiza, kupaka, kuchoma sindano au kuchanja. Madhara vile vile hutegemea kiasi cha dawa, maandalizi yake, umri wa mgonjwa, jinsia, maumbile ya vinasaba na aina ya magonjwa aliyonayo. Mfano kama una matatizo ya figo na ini, ni rahisi sana kudhurika kwa mwingiliano wa utendaji wa dawa. Mifano ya dawa zinazoingiliana Vitunguu saumu huingiliana na dawa za kupunguza makali ya VVU kama vile Ritonavir na Saquinavir Vitunguu saumu hupunguza nguvu ya dawa hizi kiasi kwamba mgonjwa anaweza kuwa na virusi vyenye usugu wa dawa hizo Vitunguu swaumu, tangawizi, mbegu na majani ya mpapai pamoja na bizari pia huongeza hatari ya mwili kushindwa kugandisha damu vinapotumiwa pamoja na dawa za hospitali.
Hii ni kutokana na kufanya damu kuwa nyepesi. Mshubiri (Aloe vera) unapotumiwa pamoja na dawa za moyo aina ya digoxin, huongeza hatari kwenye moyo kutokana na dawa hiyo asili kuwa na kawaida ya kuondoa madini ya potassium mwilini. Mshubiri una uwezo wa  kusababisha mtu kupata choo laini au kuharisha na kupoteza madini ya potassium. Ili moyo ufanye kazi vizuri unahitaji kiasi cha kutosha cha potassium.
Dawa za asili zitokanazo na Chamomile na Mpasheni zinaweza kuingiliana na dawa za usingizi za hospitalini na kuongeza hatari kwani nazo hufanya kazi ya namna hiyo. Dawa nyingi za asili zinaweza kuingiliana kiutendaji na dawa za kisukari, uzazi wa mpango na viuavijasumu. Hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari kabla ya hatari. Jinsi ya kupunguza hatari Unapotumia dawa za asili ni vema kujua aina ya mimea iliyotumiwa kutengeneza dawa hizo. Unapotumia dawa za asili, anza na kiasi kidogo na kuongeza kwa kadiri unavyoona kuwa inafaa. Pia dawa za asili na za hospitalini zinapotumiwa sambamba ni bora kuachanisha muda wa kumeza au kutumia angalau kwa saa 3 hadi 4. Jambo jingine ambalo ni la msingi sana ni kumwambia daktari kama unatumia dawa za asili kabla hujapewa dawa za hospitalini.
 Ni busara kusimamisha dawa za asili siku 7 hadi 14 kabla ya kufanyiwa upasuaji, kujifungua au kung’oa jino. Hi ini kwa sababu baadhi ya dawa za asili hupunguza uwezo wa damu kuganda, hali ambayo ni hatari wakati wa upasuaji kwani damu inaweza kuvuja bila kikomo na kusababisha kifo. Lakini pia dawa zingine huingiliana na dawa za nusu kaputi na ganzi, jambo ambalo ni hatari kwa afya na maisha wakati wa upasuaji. Majani ni mmoja wa wataalamu katika Kituo cha utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Mbeya (NIMR-MMRC 0784 688 409
Stori na Clifford Majani, Mwananchi




0 comments:

Post a Comment

MWENYEKITI WA TRAMEPRO BWANA SIMBA ABDULRAHMAN SIMBA AKITOA SALAM ZA PONGEZI KWA MHE. DKT JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI KWA KUCHAGULIWA KUWA RAISI WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SEND EMAIL TO TRAMEPRO

Name

Email *

Message *