
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi
Mussa (kushoto), Makamu wa Rais Dk. Ghalib Bilal na Mufti Shaaban Bin
Simba wakiswali swala ya Iddi el Fitr kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja
jijini Dar es Salaam jana. Picha/Omar Fungo
Mjadala kuhusu katiba mpya ulitawala katika hotuba
mbalimbali zilizotolewa jana wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya Iddi El
Fitri jana huku masheikh na viongozi wa serikali wakiwataka wajumbe wa
Bunge Maalumu la Katiba kutumia weledi, uadilifu na kuepuka maslahi
binafsi ili kuhakikisha Watanzania wanapata katiba iliyo bora.
SHEIKH MKOA WA IRINGA
Akizungumza baada ya kumalizika kwa swala ya Idd El-Fitri, iliyofanyika
katika Uwanja wa Samora mjini Iringa jana, Sheikh wa Mkoa huo, Mohamed
Mgwila, alisema viongozi wa dini wanashirikiana na waumini wote kuombea
amani nchini kuhusiana na mchakato wa katiba mpya ili maslahi ya umma
yazingatiwe na siyo ya binafsi au ya chama.
“Viongozi wote wa dini hapa nchini tunahakikisha kuliombea taifa
kupatikana kwa katiba iliyo sahihi bila kuvuruga amani iliyopo,” alisema
Sheikh Mgwila.
Alisema siyo jambo jema kwa wahusika, hususan viongozi wanaoshughulikia
jambo hilo kujikita katika kutetea maslahi ya kundi au watu fulani
katika jamii, bali inatakiwa watetee maslahi ya umma, ambayo itawasaidia
kizazi hiki na kijacho.
MDHAMINI WA BAKWATA
Mdhamini wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Omary
Nzowa, alisema maadhimisho ya Sikukuu ya Idd El-Fitri yanapaswa
kuimarisha ushirikiano miongoni mwa jamii, huku akitaka kila kundi
kutumia hekima hiyo kurejesha uhusiano wao.
ISLAMIC CENTRE
Mkuu wa Kituo cha Islamic Centre, Sheikh Hassan Mohamad, aliwataka
Waislamu kutoacha ibada hata baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi
mtukufu wa Ramadhani.
SHEIKH MKOA DODOMA
Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu Shabani, amewataka wajumbe wa
Bunge hilo kuwa kitu kimoja na kuacha kuendekeza makundi na malumbano ya
kisiasa yasiyo kuwa na msingi wakati watakaporudi bungeni mapema mwezi
ujayo ili kupata katiba iliyo bora na siyo bora katiba.
Alisema hayo alipokuwa akihutubia waumini wa dini ya Kiislamu kwenye
swala ya Idd El-Fitri, iliyosaliwa katika Msikiti wa Gadafi mjini Dodoma
jana.
Sheikh Rajabu alisema wajumbe wa Bunge hilo wamekuwa wakiendekeza
malumbano yasiyokuwa na tija kwa kila mmoja kusimamia maslahi ya chama
chake na kuacha kuwa wamoja katika kuhakikisha wanapata katiba iliyo
bora.
“Kama sintofahamu hii haitakwisha, basi ni ukweli usiopingika kuwa
hakuna katiba itakayopatikana kutokana na kutokuwapo kwa umoja wa
wajumbe wa Bunge hili la Katiba,” alisema Sheikh Shabani.
Aliwataka wajumbe hao kutambua kuwa wao ni wawakilishi wa wananchi,
hivyo hawana budi kufanya maamuzi kwa kulenga maslahi ya wananchi na
siyo vyama vyao.
“Katiba hii siyo kwa ajili ya chama fulani wala kikundi fulani, hivyo
tunatakiwa kuwa makini na kuwaombea wajumbe hawa ili waweze kuachana na
malumbano ya vyama na kufanya kile walichotumwa na wananchi,” alisema.
Aliwataka Waislamu kote nchini kuendelea kuliombea taifa kuwa na utulivu
na wasiwe tayari kurubuniwa ili wawe chanzo cha uvunjifu wa amani
iliyopo nchini.
Hata hivyo, aliwasihi waumini wa dini hiyo kuutumia mfungo wa mwezi wa
Ramadhani kuwa semina kwao ya kufanya mambo mema siku zote za maisha
yao.
“Siyo leo Ramadhani inaisha basi iwe ndiyo tumefungulia maovu yetu
tuliyoyaficha katika mwezi, ambao umeonekana kuwa na utulivu wa hali ya
juu baa zimekuwa na utulivu kana kwamba sisi Waislamu ndiyo inaoneka
tumekuwa wanywaji sana,” alisema.
SHEIKH ZUBERI
Sheikh Ahmed Zuberi aliwataka Watanzania kuendelea kuijenga na kuilinda
amani isichafuliwe na wanasiasa, ambao watapita na vyama vyao vitapita.
Aliwataka wanasiasa kuchunga kauli zao wanazozitoa kwa wananchi wakati
wakiongea nao, kwani zinaweza kuleta machafuko.Alisema maeneo yenye
machafuko kwa sasa katika maeneo mengi yanasababishwa na watu kutaka
madaraka kwa nguvu hata kufikia wakati kuvunja amani iliyopo.
SHEIKH WILAYA DODOMA
Sheikh wa Wilaya ya Dodoma, Mohamed Ramadhani aliwataka Waislamu nchini
kudumisha amani wakati wote na kuepuka ushawishi kutoka kwa watu
wasioitakia mema nchi
Akizungumza mjini Dodoma katika swala ya Idd El-Fitri, iliyofanyika
kiwilaya katika Msikiti wa Jailan, Sheikh Ramadhan alisema Watanzania
wamepewa neema na Mwenyezi Mungu ya amani, ambayo nchi nyingine
ulimwenguni hazina.
“Watanzania wenzangu tuendeleze amani yetu tuliyonayo. Wote Wakristo kwa
Waislamu tujiepushe na vurugu, ambazo zinaweza kuiingiza nchi yetu
katika machafuko ili kuendelea na amani na kufanya vitu kwa uhuru popote
tutakapotaka kwenda bila kupata tabu yoyote ya vurugu,” alisema Sheikh
Ramadhani.
Alisema Watanzania wanatakiwa kuilinda amani na kujiepusha na vurugu na
ushawishi, ambao wamekuwa wakipatiwa na watu wengine.Aliwataka
Watanzania kujitahidi kuimarisha amani na hasa wakati huu nchi ikiingia
katika mchakato wa katiba mpya.
Alisema waasisi wa taifa walijenga taifa katika hali ya umoja hivyo
Watanzania wanapaswa kuutunza umoja huo uliopo na kuendelea kuishi kwa
amani kama miaka yote.
“Nchi kama haina amani, wananchi wake watashindwa kuwa na uhuru wa
kuabudu kama tunavyoabudu hivi sasa ni kwa sababu ya amani tuliyo nayo.
Tukiipoteza kuirudisha kwake itakuwa ni shida,” alisema Sheikh Ramadhan.
Aliongeza: “Waislamu na Wakristo tumekuwa tukishirikiana kwa miaka mingi
sana na tumeimarisha amani yetu tukiwa pamoja hata katika mazingira
tunayoishi tunaishi tukiwa katika mchanganyiko hata mtume aliishi na
watu wasio Waislamu.”
Aliwataka Waislamu kote nchini kuendeleza kutenda mema kama walivyokuwa
katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani ili baraka za Mungu
ziendelee kuwa nao.
SHEIKH MKOA RUKWA
Sheikh wa Mkoa wa Rukwa, Rashid Akilimali, aliwashauri wajumbe wa Bunge
hilo wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kurejea bungeni ili
kuijadili rasimu ya katiba.
Alitoa ushauri huo mara baada ya kumalizika kwa sala ya Iddi El-Fitri,
iliyofanyika kimkoa, katika Msikiti Nuru, maarufu kwa jina la “Bakwata”,
uliopo katika Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.
Alisema ifike mahala Ukawa waamini kuwa kile wanachokifanya siyo sahihi kutokana na kususa kuhudhuria vikao vya Bunge hilo.
Sheikh Akilimali alisema kitendo hicho kinasababishia serikali na
wananchi hasara kubwa kutokana na kutopata katiba kwa wakati, huku fedha
nyingi zikiwa zimetumika.
IMAMU WA MSIKITI WA NURU
Awali, akitoa mawaidha katika ibada hiyo ya Idd, Imamu wa Msikiti huo,
Nassibu Masoud, aliwataka vijana wote nchini kumrudia Mungu na kuachana
na mambo ya kidunia na yale ya kuiga, ambayo wengi wao yamekuwa
yakiwasababishia madhara makubwa.
Alisema kwa sasa vijana wengi wanakosa kuishi kwa maadili kutokana na
kujiingiza katika mambo yasiyofaa na kuacha kumcha Mwenyezi Mungu.
SHEIKH MKOA ARUSHA
Viongozi wa dini ya Kiislamu mkoani Arusha wameahidi kuendelea kusaidia
kutoa ushirikiano wa kukabiliana na watu wanaopitia migongo ya
madhehebu ya dini kufanya maovu na kuwataka vijana kuwa macho na baadhi
ya watu wanaotaka kuwarubuni wakubali kutumia nguvu zao kuvuruga amani
ya nchi.
Wakizungumza baada sala ya Idd El-Fitri, viongozi hao, akiwamo shekh
mkuu wa mkoa Shaban Bin Jumaa, wamesema kimsingi wote
wanaofanya maovu kwa kupitia kwenye madhehebu ya dini siyo
waumini wa kweli kwani hakuna dhehebu la dini linaloelekeza mtu
kufanya maovu Shekh shabani amesema vitabu vyote vitakatifu
vinaonyesha kuwa lengo la madhehebu yote ya dini ni kutenda mema
na kushirikiana na kupendana na watu wote waliopokea ujumbe huo
vizuri wamekuwa wanatekeleza hilo na ni jambo lililoko wazi kuwa
wanaokwenda kinyume eidha wana agenda zao ama hawajaelewa
vizuri na wanahitaji kujifunza zaidi kwa upande wake Imamu wa
msikiti wa Ngarenaro Mahamud Suleiman Nyambwa na Imamu wa
Msikiti wa Ollmatejoo Omari Saidi wameiomba serikali kutomuonea
huruma mtu yeyote anayetaka kutumia kivuli cha dini kuvuruga
amani.
Viongozi hao wamesema kimsingi licha ya kuwapo kwa tofauti za
njia za kuabudu dini zote zinahamasisha amani upendo na
ushirikiano na wanaokwenda kinyume hawana lengo la kuabudu bali
wanaweza wakawa na agenda zao Sala ya Idd El-Fitri, ambayo kimkoa
ilifanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abedi na pia katika
misikiti mbalimbali imemalizika kwa amani na huku jeshi la
polisi likiwa limeimarisha ulinzi wa aina mbalimbali ukiwemo
wa askari kanzu na wa kawaida.
SHEIKH MKOA RUVUMA
Waumini wa dini ya Kiislamu mkoani Ruvuma wametakiwa kusherehekea
Sikukuu ya Idd El Fitri kwa amani, utulivu na upendo miongoni mwao na
jamii inayowazunguka kama ilivyoagizwa na Mwenyezi Mungu katika
mafundisho yake kwa wanadamu.
Kauli hiyo ilitolewa na Shaban Kitete wa Mkoa wa Ruvuma wakati akitoa
mawaidha kwenye Msikiti wa Mkoa wa Ruvuma uliopo mjini Songea katika
kusherehekea Sikukuu ya Idd El Fitri.
Alisema Waislamu wote nchini wanapaswa kuwa chachu ya kudumisha amani,
umoja na upendo uliopo nchini siyo tu wakati wa mfungo wa mwezi wa
Ramadhan na Sikukuu ya Idd wanapaswa kuishi hivyo katika maisha yote.
Aidha amewataka kujijengea utamaduni wa kusherehekea sikukuu hiyo kwa
kualika watu wengine bali kujali itikasi zao za kidini kwa kufanya hivyo
kunadhirisha maana halisi ya sikukuu hiyo na kutazidisha upendo na
usalama wa nchi ambao kila mmoja anauhitaji katika kuishi kwake na kamwe
wasikubali kutumiwa watu au vikundi vya watu wasiotakia mema nchi
iliyojaa amani na utulivu kwa miaka mingi.
Amesema kila Mtanzania amnapaswa kumshukuru Mungu kwa kuijalia amani
nchi kwa miaka mingi hivyo kila mmoja anapaswa kuishi katika misingi ya
kudumisha amani hiyo iliyopo ambayo ina historia kubwa ndani na nje ya
nchi ambayo inamfanya kila mmoja ajivunie kuitwa Mtanzania
ikilinganishwa na matukio ya uvunjifu wa amani yanayotokea katika
mataifa mengine ulimwenguni ambayo yanasababisha vifo kila uchao.
Akitoa mfano wa maafa hayo Shekh Shaban Kitete amelitaja tukio la hivi
karibuni ambalo ndege ya nchini Malasya imaeangushwa na kusababisha vifo
vya takribani 300 ulimwengu wote umelaani na kukemea mauaji hayo lakini
ulimwengu huo huo unashindwa kulaani na kukemea kwa nguvu mauaji
yanayofanywa na Israel kwa wananchi wa Palestina ambayo mpaka sasa idadi
yao inafikia zaidi ya mia moja.
Aidha ametoa wito kwa mataifa yote ulimwenguni kote kutumia nguvu zao
kuhakikisha ulimwengu wote unakuwa salama na wenye amani na utulivu
kwani muumini wa imani yoyote anayeweza kuabudu kama hakutakuwa na amani
ya kuwafanya wanadamu wote kuishi kama ndugu bila kujali imani na
itikadi walizo nazo kwa sababu imani zote zinamtukumza na kumuabudu
Mungu mmoja.
Akizungumzia mchakato wa katiba mpya unaoendelea Shekh Shaban amewaasa
wajunbe wa umoja wa katiba ya wananchi(UKAWA) kurejea bungeni kuendelea
na mjadala huo ili hatimaye katiba mpya itakayowasaidia watanzania wote
kuishi kwa amani na kujiletea maendeleo yao iweze kupatikana na amesema
kuwa kama UKAWA wanasusia bunge hilo kwa maslahi na mustakabali mwema wa
nchi Mungu awabariki lakini kama ni kwa maslahi yao binafsi na ya
kisiasa Mungu atawahukumu.
Amewaasa wanasiasa wote chini kudumisha amani,upendo na utulivu kwa
kutumia utamaduni wa kujadiliana na kuridhiana katika masuala yote
yaliyo na utata kwa mustakabali wa nchi kama ulivyorithishwa kwa wazee
wa taifa hili na siyo kulumbana na kukashifiana kwani huo siyo utamaduni
wa watanzania.
PINDA
Akizungumza katika Baraza la Iddi lililofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond
Jubilee jijini Dar es Salaam jana, Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliwasihi
wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuacha kususia
vikao vya Bunge la Katiba na kurejea bungeni ili wapate nafasi ya
kuzungumza tofauti zao na kuzimaliza kwa nia ya kunusuru mchakato wa
kuundwa kwa katiba mpya.
Akieleza zaidi, Pinda alisema kuwa kiutaratibu, ndani ya Bunge Maalum la
Katiba kuna Kamati ya Mashauriano ambayo inaweza kumaliza mabishano au
tofauti zozote zilizojitokeza baina yao.
Ukawa huwahusisha wajumbe wengi kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi.
Hii siyo mara ya kwanza kwa Waziri Mkuu Pinda kuwasihi wajumbe wa Ukawa kurejea bungeni.
Aliwahi pia kutoa kauli kama hiyo mkoani Kilimanjaro wakati akiweka jiwe
la msingi katika Chuo cha Ufundi Gonja/Mheza, kilichopo katika Wilaya
ya Same, akisisitiza kuwa ni vyema wakarejea na kuzungumza ili
wasameheane pale walipokosea na kuwezesha mchakato wa kuundwa kwa katiba
kuendelea.
Bunge hilo maalum la katiba linatarajiwa kuanza tena Agosti 5, lakini
hadi sasa, uwezekano wa wajumbe wa Ukawa kurejea bungeni ni mdogo kwani
viongozi wao, wakiwamo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake
wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na James Mbatia wa NCCR - Mageuzi
wamekuwa wakisisitiza kuwa hawatarejea bungeni hadi watekelezewe
masharti yao.
Ukawa waliamua kutoka bungeni na kuwaacha wajumbe wengi walio wafuasi wa
Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya kupinga jaribio la kubadili rasimu
iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji
mstaafu Joseph Warioba, ambayo imeonyesha kuwa maoni ya wananchi
yakitaka muundo wa muungano wa serikali tatu.
Wajumbe wanaoiunga mkono CCM wamekuwa wakipinga maoni hayo ya Tume ya
Warioba na kutaka kuendelea kuwapo kwa muundo wa muungano wa serikali
mbili lakini uliofanyiwa mabadiliko makubwa.
Imeandikwa na Thobias Mwanakatwe (Dar), George Tarimo (Iringa), Paul
Mabeja (Dodoma), Furaha Eliab (Mbeya), Juddy Ngonyani na Arafa Masingo
(Sumbawanga), Asraji Mvungi (Arusha), Rahma Suleiman (Zanzibar) na
Natha Mtega (Songea).