Kama
mnavyofahamu, Serikali inatambua umuhimu wa Tiba Asili ambayo ni tiba kongwe
zaidi nchini, imekuwepo toka enzi na enzi. Pia, watanzania zaidi ya asilimia
sitini (60%) wanatumia huduma hii ya Tiba Asili. Hivyo, ni muhimu kuhakikisha
kuwa inaboreshwa na kuendelezwa ili kupanua wigo wa watumiaji, huku tukiwa na
uhakika wa ubora na usalama wa huduma hii. Katika kutekeleza hayo, Serikali
imerasimisha Tiba Asilia kwa kujumuisha Tiba Asili na tiba Mbadala kwenye Sera
ya Afya pamoja na kutunga Sheria.
Ndugu Wananchi,
Baraza
la Tiba Asili na Tiba Mbadala lilianzishwa kisheria chini ya Sheria ya Tiba
Asili na Tiba Mbadala Na.23 ya Mwaka 2002, kwa lengo la kusimamia, kudhibiti na
kuendeleza huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini. Baraza lilizinduliwa
rasmi mwaka 2005.
Usajili
wa Waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala, Wasaidizi na vituo vya kutolea huduma
ulianza rasmi mwaka 2011. Hadi sasa Baraza limefanikiwa kusajili waganga zaidi
ya elfu kumi na nne (14,000) na vituo mia moja na themanini (180).
Ndugu Wananchi,
Pamoja
na mafanikio hayo, Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kwa kushirikiana na
taasisi mbalimbali za Serikali limeweka mfumo unaoweza kuwasaidia walaji
kuhakikisha kuwa wanatumia dawa za asili
zilizo salama kwa kuzipima katika maabara zinazotambulika na Serikali. Dawa
zitakazopimwa zitawawezesha waganga kusajili dawa zao, na hivyo kuwasaidia kufanya
kazi kwa kujiamini na kupata soko ndani na nje ya nchi na kuongeza kipato chao
binafsi na kwa Taifa.
Ndugu Wananchi,
Usajili
wa dawa za tiba asili utategemea vigezo vifuatavyo:
·
Mtaalamu wa tiba asili lazima awe
amesajiliwa kisheria na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na ana leseni ya
kufanyia kazi iliyo hai.
·
Kituo cha kutolea huduma lazima kiwe
kimesajiliwa na kina leseni iliyo hai. Sehemu ya kuzalishia dawa iwe
imekaguliwa na kuthibitika kuwa inafaa kwa kuzalishia dawa.
·
Mtaalamu wa tiba asili anapaswa kuwasilisha
katika Ofisi ya Msajili wa Tiba Asili na Tiba Mbadala, taarifa sahihi za
uchunguzi wa dawa yake kutoka katika taasisi zilizoainishwa katika fomu ya
usajili wa dawa. Taasisi hizo ni BRELA, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mabaara
ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Taasisi ya Chakula na Lishe, Maabara ya Taifa ya
Afya, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi na Taasisi ya Taifa ya Utafiti
wa Magonjwa ya Binadamu.
Serikali
linawaasa waganga wa tiba asili na tiba mbadala wote kufuata sheria na
kuhakikisha kuwa dawa zinaandaliwa kwa ubora na zinasajiliwa kwa mujibu wa sheria
ili kuinua tiba asili nchini. Naliagiza Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala
kusimamia suala hili kikamilifu.
Kwa
kusema hayo nazindua rasmi usajili wa dawa za tiba asili leo tarehe 24/11/2016.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
0 comments:
Post a Comment