NA MWANDISHI WETU, Dar
ALIYEKUWA
Katibu Mkuu wa Shiririka la Kusaidia Wazee, Tumaini la Wazee Tanzania,
(TUWATA) jijini Mbeya, Dk. David Magogo, anatarajiwa kuzikwa leo katika
Makaburi ya Uwanja wa Sababasaba jijini humo.
Dk.
Mgogo ambaye pia ni mwasisi wa shirika hilo alifariki dunia juzi saa
saba mchana katika Hospitali Teule ya Ifisi, nje kidogo ya Jiji la Mbeya
alikokuwa amelazwa kwa
matibabu.
Msemaji
wa TUWATA, Boniventure Mwalongo, aliliambia Raia Tanzania jana jijini
Dar es Salaam kuwa, marehemu kwa muda mrefu alikuwa akisumbuliwa na
ugonjwa wa moyo na tatizo la mfumo wa upumuaji.
“Hivi
karibuni alionekana kama afya yake imetengamaa kwa sababu mimi nilikuwa
Mbeya siku mbili zilizopita na nilizungumza naye mara kadhaa, lakini
kumbe ndio alikuwa kama anatuaga,” alisema Mwalongo.
Mwalongo
alisema moja ya mambo ambayo yatawafanya wamkumbuke ni kuasisi shirika
hilo kwa ajili ya kuwasaidia wazee jijini Mbeya na mikoa ya jirani.
“Baada
ya kustaafu aliamua kuanza jitihada za kuunda
chombo cha kuwasaidia wazee na hatimaye alifanikiwa kuunda TUWATA
ambayo awali, kabla ya usajili, ilifahamika kama Saidia Wazee. Hili
ndilo jambo kubwa ambalo ameliacha na atakumbukwa daima,” alisisitiza.
Akizungumza
kwa njia ya simu kutoka Mbeya, Mwenyekiti wa TUWATA, Lydia Njeni,
alisema Dk. Magogo ameacha pengo, huku akisisitiza serikali kutowasahau
wazee katika suala la matibabu wanapokumbwa na
maradhi.
“Dk.
Magogo kwa umri wake alikuwa mzee, kweli aliugua kwa muda mrefu na hadi
anafariki dunia, nilikuwa naye kwa karibu sana. Ni kama amefia mikononi
mwangu. Tatizo lililoko hapa ni gharama kubwa za matibabu kwa wazee
kama sisi.
“Kwa
mfano, hata ile juzi baada ya kufariki dunia, tukampeleka katika chumba
cha kuhifadhia maiti, tukaambiwa tutoe Sh 40,000. Jamani fedha hizi
tunazipata wapi sisi wazee? Naona bado Serikali imetusahau sana wazee,”
alisema Lydia.
Mratibu
wa asasi zisizo za kiserikali katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya,
Victor Kabuje, alisema atamkubuka Dk. Magogo kama mtu aliyekuwa na
ubunifu wa kipekee na hasa katika suala la kuwasaidia watu.
“Mimi
nakumbuka jinsi alivyokuja
kwangu na tukashirikiana kuisajili TUWATA, baada ya hapo akanipa
uanachama wa heshima. Kila wakati alikuwa mtu wa kuja na mawazo mapya,”
alisema Kabuje.
Katika
hatua nyingine, mtoto wa marehemu, Joyce Magogo, aliwashukuru watu wote
waliotoa michango yao ya hali na mali katika msiba wa baba yake.
Dk.
Magogo alizaliwa April 2, 1934 wilayani Korogwe, Tanga. Alikuwa na
taaluma ya udaktari wa binadamu. Katika nyakati tofauti alifanya kazi
katika hospitali za Bugando Mwanza, Kwimba, Tukuyu, Kyela na Mbeya kabla
ya kustaafu mwaka 1992.
Ends.