Wakati mwingine mwingiliano kinzani wa kiutendaji wa dawa za
asili na zile za hospitalini, unaweza kusababisha dawa kugeuka kuwa sumu na kusababisha mzio hatari wa kuzimia na kushindwa kupumua.
Watu wanaougua
magonjwa sugu wamekuwa wakijikuta kwenye mkanganyo kiasi cha kuwafanya watumie
dawa za hospitalini pamoja na zile za asili bila kujua athari mbaya zaidi
zitakazowapata. Matumizi ya dawa za asili au tiba mbadala kwa sasa yameenea
sana. Za asili zinajizolea umaarufu sehemu mbalimbali duniani kutokana na
kupigiwa debe muda mwingi
Sheria za kimataifa zinapiga marufuku dawa za hospitalini
kutangazwa kwa sababu mwenye mamlaka ya kuamua matumizi ni daktari na wala si
mgonjwa Dawa za hospitalini hadi ziidhinishwe kwa matumizi ni lazima zipitie
hatua mbalimbali kuthibitisha viwango vya kutibu, faida na hasara. Dawa za
asili zimekuwa zikitumika ama kutokana na mazoea au mgunduzi kuzitangaza wakati
athari zake zinazotokana na kiwango cha sumu kilichopo kutokujulikana.Pamoja na
hali hiyo, jambo la hatari zaidi ni watu wengi kuchanganya dawa hizi za asili
na zile zinazotengenezwa maalumu kutolewa hospitalini.Wagonjwa wengi hasa wenye
magonjwa sugu yanayoelekea kushindikana hospitalini wanatumia tiba za asili
kubahatisha uwezekano wa kupona. Wengine kwa kutokujiamini hujikuta wanaenda
hospitali kupata dawa na wakati huo huo huenda kwa waganga wa jadi kupata
huduma.Wengine wanapokwenda kuonana na madaktari, huwa hawako tayari kuweka
wazi kwamba wanatumia dawa nyingine za asili.Kuna baadhi ya waganga wa jadi,
kwa tamaa zao huwa wanawaambia wateja wao kuwa dawa zao haziwezi kuingiliana na
zile za hospitali kwa kuwa ni kama chakula tu.
Ukweli ni kwamba nyingi zina sumu.Taarifa nyingi za kitabibu
za hivi karibuni zinaonyesha kuwa wapo watu wengi wanaochanganya dawa hizi na
kujikuta wanatengeneza tatizo jingine ambalo pengine ni kubwa zaidi ya lile
linalowasibu.Katika utafiti huo, inaonekana kwamba madhara ya mwingiliano ama
ukinzani wa dawa za asili na zile za kisasa, linaongezeka.Hata hivyo, taarifa
hizi zinaweza kuwa hazitoi picha kamili kwa vile takribani asilimia 70 ya
wagonjwa walioathirika, hawaelezi ukweli wa kuchanganya dawa.Kwa sababu hiyo
hakuna utaratibu maalumu wa kuweka takwimu ili kufuatilia ukubwa wa tatizo
hilo.
Dk Shufeng ZHOU aliandika makala kwenye jarida la ‘Herbal
Medicine Drug Interactions’ nchini
Singapore, toleo la 6, akielezea juu ya utafiti wa matumizi mchanganyiko wa
dawa za asili na zile za hospitalini.Dk Zhou anasema matumizi ya namna hiyo
yanaweza kusababisha mwingiliano au ukinzani wa dawa na kusababisha madhara
makubwa kwa mtumiaji.Matumizi ya namna hii yanaweza kuzuia dawa moja isifanye
kazi, au moja iwe na nguvu zaidi kuliko kawaida na kudhuru mwili.Dawa zote
zinaweza kujishikiza katika vipokeleo vya dawa vya aina moja na kushindana au
kuzuia uzalishaji wa vimeng’enyo vya mwili visisafirishe dawa mwilini kama
inavyotakiwa.Hali ya namna hii inaweza kusababisha usugu wa viini vya magonjwa
hatari dhidi ya dawa mfano Viini vya Kifua Kikuu (TB), Virusi Vya Ukimwi (VVU),
au kudhurika kwa ini na figo na kusababisha viungo hivi vya mwili, kushindwa
kufanya kazi zake vizuri. Wakati mwingine mwingiliano kinzani wa kiutendaji wa
dawa za asili na zile za hospitalini, unaweza kusababisha dawa kugeuka kuwa
sumu na kusababisha mzio hatari wa kuzimia na kushindwa kupumua.Hatari ya
mwingiliano kinzani wa utendaji wa dawa, huwa mkubwa zaidi pale dawa zaidi ya
moja zinapotumiwa kwa pamoja.Mtafiti mmoja wa maswala ya dawa anasema kuwa, mtu
anapotumia dawa mbili kwa wakati mmoja, hatari ya mwingiliano kinzani ni
asilimia 6. Anapotumia aina tano za dawa mwingiliano ni asilimia 50 na hatari
huongezeka zaidi hadi kufikia asilimia 100 pale mtu anapochanganya dawa nane au
zaidi.
Hii ni kwa mujibu wa Kuhn Merrily, katika kitabu chake cha
“Pharmacotherapeutics: A Nursing Process Approach. Philadelphia, Pa: FA Davis,
1998”.Dawa zinapoingiliana kiutendaji, hutengeneza mazingira yasiyofaa katika
tumbo la chakula na utumbo, kiasi kwamba sehemu hizi za mwili hushindwa kufanya
kazi ipasavyo. Matokeo yake ni kuharisha, kupata kichefuchefu au kupata vidonda
vya tumbo au mwili kushindwa hufyonza kiasi cha kutosha cha dawa kwa ajili ya
kupambana na ugonjwa. Mfano mzuri ni pale mtu anapotumia aloe vera na dawa za
hospitalini kwa wakati mmoja anaweza kuharisha.
Pia mwingiliano
kinzani unaweza kusababisha dawa kujishikiza katika vipokeleo visivyo vya
kawaida na kushindwa kusambaa kama inavyotarajiwa. Tatizo jingine hutokea
wakati dawa zilizoingiliana kiutendaji zinapofika ndani ya ini. Hapo dawa
huathiri vimeng’enywa vya ini vinavyoshughulikia dawa, vijulikanavyo kama CYP
450 enzymes na P-glycoprotein. Hali hii huweza kupunguza au kuongeza makali ya
dawa kwa namna isiyokuwa ya kawaida.Hatari haiishii hapo, dawa zinapoingiliana kiutendaji
pia huathiri utendaji wa figo na kushindwa kuondosha kiasi kikubwa cha sumu
hatari mwilini. Hali hii inaweza kudhuru figo na kusababisha kiungo hicho
muhimu kufa au kuwa dhaifu kiutendaji. Mwingiliano wa Dawa tunazotumia huathiri
miili yetu kwa wema au kwa ubaya. Dawa zinapoingiliana kiutendaji zinaweza
kupingana au kuongezeana nguvu na kuleta ufanisi au kuongeza makali ya dawa na
kuwa sumu. Baadhi ya dawa za asili
zitokanazo na mimea huongeza makali ya dawa za hospitalini na nyingine
hupunguza makali yake na kuvuruga kazi iliyokusudiwa ya kupambana na vimelea
vya magonjwa Dawa za hospitalini pia huweza kuingiliana na zile za kufukiza,
kupaka, kuchoma sindano au kuchanja. Madhara vile vile hutegemea kiasi cha
dawa, maandalizi yake, umri wa mgonjwa, jinsia, maumbile ya vinasaba na aina ya
magonjwa aliyonayo. Mfano kama una matatizo ya figo na ini, ni rahisi sana
kudhurika kwa mwingiliano wa utendaji wa dawa. Mifano ya dawa zinazoingiliana
Vitunguu saumu huingiliana na dawa za kupunguza makali ya VVU kama vile
Ritonavir na Saquinavir Vitunguu saumu hupunguza nguvu ya dawa hizi kiasi
kwamba mgonjwa anaweza kuwa na virusi vyenye usugu wa dawa hizo Vitunguu
swaumu, tangawizi, mbegu na majani ya mpapai pamoja na bizari pia huongeza
hatari ya mwili kushindwa kugandisha damu vinapotumiwa pamoja na dawa za
hospitali.
Hii ni kutokana na kufanya damu kuwa nyepesi. Mshubiri (Aloe
vera) unapotumiwa pamoja na dawa za moyo aina ya digoxin, huongeza hatari
kwenye moyo kutokana na dawa hiyo asili kuwa na kawaida ya kuondoa madini ya
potassium mwilini. Mshubiri una uwezo wa kusababisha mtu kupata choo
laini au kuharisha na kupoteza madini ya potassium. Ili moyo ufanye kazi vizuri
unahitaji kiasi cha kutosha cha potassium.
Dawa za asili zitokanazo na Chamomile na Mpasheni zinaweza
kuingiliana na dawa za usingizi za hospitalini na kuongeza hatari kwani nazo
hufanya kazi ya namna hiyo. Dawa nyingi za asili zinaweza kuingiliana
kiutendaji na dawa za kisukari, uzazi wa mpango na viuavijasumu. Hivyo ni
muhimu kuchukua tahadhari kabla ya hatari. Jinsi ya kupunguza hatari Unapotumia
dawa za asili ni vema kujua aina ya mimea iliyotumiwa kutengeneza dawa hizo.
Unapotumia dawa za asili, anza na kiasi kidogo na kuongeza kwa kadiri unavyoona
kuwa inafaa. Pia dawa za asili na za hospitalini zinapotumiwa sambamba ni bora
kuachanisha muda wa kumeza au kutumia angalau kwa saa 3 hadi 4. Jambo jingine
ambalo ni la msingi sana ni kumwambia daktari kama unatumia dawa za asili kabla
hujapewa dawa za hospitalini.
Ni busara kusimamisha
dawa za asili siku 7 hadi 14 kabla ya kufanyiwa upasuaji, kujifungua au kung’oa
jino. Hi ini kwa sababu baadhi ya dawa za asili hupunguza uwezo wa damu
kuganda, hali ambayo ni hatari wakati wa upasuaji kwani damu inaweza kuvuja
bila kikomo na kusababisha kifo. Lakini pia dawa zingine huingiliana na dawa za
nusu kaputi na ganzi, jambo ambalo ni hatari kwa afya na maisha wakati wa
upasuaji. Majani ni mmoja wa wataalamu katika Kituo cha utafiti wa Magonjwa ya
Binadamu Mbeya (NIMR-MMRC 0784 688 409
Stori na Clifford Majani, Mwananchi